IGP SIMON SIRRO ASEMA HALI YA USALAMA NCHINI NI SHWARI NA HAKUNA MATUKIO YA KUTISHA


Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro amesema hali ya usalama nchini ni shwari, na hakuna matukio ya kutisha.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo katika Chuo Cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam,  baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua kiwanda cha ushonaji cha Jeshi la Polisi.

Amesema kuna matukio madogo ya uhalifu ambayo yamekuwa yakitokea katika maeneo mbalimbali nchini, ambayo Jeshi la Polisi nchini limekuwa likikabiliana nayo.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini amesema matukio ya uhalifu nchini yameendelea kupungua, na kutolea mfano katika kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili mwaka huu yamepungua kwa zaidi ya asilimia 13 tofauti na ilivyokuwa katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Amesema katika kipindi hicho hicho, pia ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 29.1.

Kwa mujibu wa IGP Sirro, Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ndani na nje ya nchi, linaendelea kupambana na vitendo vya ugadi na biashara ya dawa za kulevya.

Kuhusu nidhani ndani ya Jeshi la Polisi, IGP Sirro amesema ni ya kuridhisha na askari ambao wamekuwa wakikiuka sheria wanachukuliwa hatua za kinidhamu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post