Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mjini Kahama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema inadaiwa kuwa tarehe 14/12/2020 majira ya saa 02:00 usiku katika kijiji cha Mawemilu Tarafa ya Nindo Wilaya ya Shinyanga Vijijini na Mkoa wa Shinyanga Hadija Kisina Holo akiwa ndani ya nyumba yake aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na watu wasiofahamika.
"Mara baada ya tukio hili kutokea upelelezi ulifanyika na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa Shinje Ngula (23) na Kisinza Lusamila (28) mnamo tarehe 19/05/2021 huko Mpanda Mkoani Katavi kufuatia msako mkali uliofanywa na kikosi kazi cha Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa",amesema Kamanda Magiligimba.
Ameeleza kuwa watuhumiwa wamekiri kuhusika na mauaji hayo na taratibu za upelelezi zinaendelea na zitakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga anatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa dhidi ya watuhumiwa wengine waliohusika kwenye tukio hilo la sivyo wajisalimishe wenyewe kwani watakamatwa tu.
Social Plugin