MAJALIWA: WATAFITI, WABUNIFU ONGEZENI KASI YA TAFITI
الاثنين, مايو 24, 2021
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watafiti na wabunifu nchini kuongeza kasi ya kufanya tafiti ili nchi iende sambamba na mabadiliko yanayotokea ulimwenguni kote.
Ametoa wito huo leo Mei 24, 2021 wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya sita ya wiki ya utafiti na ubunifu yakiyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jijini Dar es Salaam.
“Mabadiliko haya ya teknolojia yanatokea kwa kasi kubwa ulimwenguni yanachochewa na mwenendo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hivyo basi, nasi hatunabudi kujipanga vyema ili kuendana na kasi hiyo”.
Amesema kuwa ni lazima watafiti na wabunifu katika sekta zote wachukue hatua za makusudi katika kubuni na kutumia teknolojia zinazoibuka kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu ya viwanda na jamii yetu.
“Wakati tukifanya hayo yote, ni muhimu pia kujitayarisha kutumia kikamilifu matokeo ya tafiti zetu kama fursa au bidhaa adimu ya biashara”
Aliongeza kuwa baada ya tafiti hizo wahakikishe matokeo ya tafiti yanapelekwa kwa umma ili uweze kufaidika na matokeo hayo kwa kupata suluhisho za changamoto mbalimbali zinazoikabili Jamii badala ya kuyafungia makabati.
Aidha, Waziri Mkuu amevitaka vyuo vikuu vyote nchini kuweka utaratibu wa kufanya utafiti na kisha kuonesha matokeo ya tafiti ili kusaidia kuimarisha uhusiano wa karibu baina ya vyuo na soko la ajira.
Kadhalika Waziri Mkuu ametoa wito kwa wenye viwanda kutoa ufadhili wa tafiti na bunifu zinazohusiana na bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vyao.
“Tumieni vizuri wataalamu wa vyuo vyetu kwani wanaweza kuleta majibu ya changamoto mbalimbali katika uzalishaji bidhaa, masoko ya bidhaa, mahitaji ya wateja na mambo mengine mengi”
Pia, Waziri Mkuu amekitaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutekeleza mpango wa vitengo vya utafiti kwenye mikoa ikiwemo cha mkoa wa Lindi ambako tayari walikwisha pewa eneo.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha tafiti ili taifa liweze kunufaika na teknolojia ya kisasa na kutoa huduma kwa jamii.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin