Waziri wa Maji nchini Tanzania Jumaa Aweso amesema watazichukulia hatua mamlaka zote ambazo zitabainika kuwabambikizia bili wateja wa maji nchini.
Aweso ameyasema hayo jana Jumatatu Mei 10, 2021 wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaa wa fedha 2021/2022.
Alisema jukumu la wizara ni kuhakikisha kuwa mwananchi habambikiwi bili za maji
“Niwapongeze wabunge kwa kuwasilisha malalamiko ya wananchi wao, hata mimi nilipopita huko nimesikia malalamiko hayo. Ni kweli anayelala na mgonjwa ndio anajua mihemo ya mgonjwa,” alisema.
Alisema baada ya kusikia malalamiko hayo wametoa maagizo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati (Ewura) kufuatilia malalamiko hayo.
“Wameshafanyia kazi nataka niwadhibitishie wabunge mamlaka yoyote itakayokuwa imekwenda kinyume aidha kwa kuwabambikizia bili wateja au kutoa bili ambazo hazijaidhinishwa na Ewura tutazichukulia hatua hata ziwe na mapembe kiasi gani,” alisema.