MGOMBEA UBUNGE BUKOBA MJINI KUPITIA CHADEMA CHIEF KALUMUNA NA WENZAKE WAACHIWA HURU

 

Chief Kalumuna akiwa eneo la Mahakama jana kwa ajili ya kusikiliza hukumu ya kesi iliyokuwa ikimkabili

Na Ashura Jumapili, Bukoba
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Bukoba imewaachia huru washtakiwa saba akiwemo Aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba na aliyekuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukoba mjini kupitia Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Chief Kalumuna baada ya kuwakuta hawana hatia katika kesi ya jinai iliyokuwa ikiwakabili.

Katika kesi hiyo namba 257 ya mwaka 2020, washtakiwa wengine walioachiwa huru ni Ismail Kamala, Antidius Mutajoa, Abdumalik Audax, Jovitus Rwebangaiza, Victor Sherejei na Sostenesi Mutashoberwa wote wakazi wa manispaa ya Bukoba.

Chief Kalumuna na wenzake walikuwa wanatuhumiwa kwa makosa nane yakiwemo ya kusababisha fujo, kutotii, kusababisha uharibifu wa mali na kusababisha majeraha siku ya kuwaapisha mawakala wa Vyama vya Siasa tarehe 21 mwezi wa 10 mwaka 2020.

Ambapo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Bukoba, Joseph Lwambano amesema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuthibitishwa hivyo inaonyesha washtakiwa hawakuhusika.

Akisoma uamuzi wa kesi hiyo, Hakimu Mkazi Mahakama ya Bukoba, Joseph Luambano alisema kutokana na ushahidi uliomo katika kesi hiyo mahakama inashawishika kusema kwamba watuhumiwa walishtakiwa kwa hisia kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa kuithibitishia mahakama bila kuacha shaka kuwa washtakiwa walitenda makosa waliyoshtakiwa nayo.

‘’Ninapata ugumu kumuelewa shahidi namba tano ambaye ni msimamizi wa uchaguzi jimbo la Bukoba mjini, Morice Limbe alitumia sheria gani au alifanya hayo kwa mamlaka ipi.....Yule aliyepewa dhamana hiyo ni lazima afanye hivyo kwa misingi ya sheria pasipo kuingiza mambo yake binafsi katika vitu ambavyo tayari vinatekelezwa kisheria,” alisema hakimu Luambano.

Hakimu Luambano ameeleza kuwa mahakama inalazimika kuamini kwamba wale watu nje ya washtakiwa walijiongoza vibaya kwenye kutekeleza majukumu yao, hivyo hakuna mazingira ambayo mtu anaruhusiwa kutumia Sheria mkononi.

Mkuu wa Mashtaka mkoa wa Kagera, Basilius Namkambe, alisema wataipitia hukumu kuangalia na kuitafakari kuona kama wanaweza kukata rufaa

“Tutafanya hivyo tukishapewa nyaraka zote mahakamani kwa sababu tunao muda kisheria wa kufanya hivyo,” alisema.

Namkambe, alisema wajibu wao ilikuwa kupeleka kesi mahakamani na ushahidi hakimu amekaa katikati na kuona ushahidi haujajitoleza upande wa Jamhuri hivyo watapitia tena hukumu na kuona kama watakata rufaa ama la.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post