Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Monsinyo Msimbe alikuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro.
Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., alizaliwa tarehe 27 Desemba 1963 huko Homboza, Jimbo Katoliki la Morogoro.
Baada ya masomo yake ya msingi na sekondari, alijiunga na masomo ya falsafa kwenye Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi.
Baadaye aliendelea na masomo ya taalimungu, Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Baada ya majiundo yake ya kitawa, tarehe 8 Desemba, 1987, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, akaweka nadhiri zake za daima na hatimaye, kupewa daraja Takatifu ya Upadre tarehe 21 Juni 1998.
Askofu mteule Msimbe aliendelea na masomo ya juu kwenye Chuo kikuu cha “Heythrop College” huko London, Uingereza na kujipatia Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kanisa kutoka katika Chuo Kikuu cha Uingereza.
Baadaye pia alijiendeleza na hatimaye kujipatia shahada kwenye Sheria za Kimataifa kutoka katika Chuo Kikuu cha West-England, kilichoko Bristol, Uingereza.
Baada ya kurejea nchini Tanzania, alipangiwa utume wa kuwa ni mlezi wa Wapostulanti na Wanovisi wa Shirika la Mungu Mwokozi, maarufu kama Wasalvatoriani. Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2012 alichaguliwa kuwa Padre Mkuu wa Kanda ya Shirika la Mungu Mwokozi, nchini Tanzania.
Baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, ameendelea kuwa ni mlezi wa Shirika kimataifa katika nyumba ya malezi "Mater Salvatoris" iliyoko Jimbo Katoliki la Morogoro.Tarehe 13 Februari 2019 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro.
Tarehe 30 Desemba 2020 akateuliwa tena kuwa Msimamizi wa Kitume “Sede Vacante ad nutum Sanctae Sedis” Jimbo Katoliki la Morogoro. Yaani kama Msimamizi wa Kitume, alikuwa anawajibika moja kwa moja na Vatican katika masuala yote ya uongozi wa Jimbo Katoliki la Morogoro.
Social Plugin