Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Salim Kali, ameagiza kuhamishwa wilayani kwake mwalimu anayetuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi watatu wa kike wa shule ya msingi ya Ilungu katika kitanda kimoja.
Mwalimu huyo aliyetajwa na Mkuu wa wilaya kwa jina la Martin Mambosasa anadaiwa kufanya vitendo hivyo kwa nyakati tofauti kwa miaka saba.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema mwalimu huyo aliwahi kukamatwa na vyombo vya dola na kufikishwa mahakamani, lakini akahonga wazazi wa watoto hao wakaharibu ushahidi.
Alitoa agizo hilo juzi kwenye kongamano la kuweka mikakati ya kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, mimba katika umri mdogo na utoro kwa wanafunzi.
Alisema mikakati hiyo itasaidia kuongeza ufaulu na kwamba mwaka 2020, takwimu zinaonyesha matukio ya ukatili wa kijinsia yalikuwa 304.
Alimuagiza mratibu Elimu wa kata na ofisa elimu wa wilaya kumhamishia mwalimu huyo sehemu nyingine Ili asionekane wilayani kwake.
"Huyu mwalimu amekuwa akidhalilisha watoto wadogo kwa kipindi kirefu na naagiza ahamishwe sitaki kumsikia wala kumuona hapa wilayani kwangu," alisema
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Magu, Amandus Mboya alisema mambo yanayochangia ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia ni pamoja na wazazi kushindwa kuwapatia huduma muhimu.
Alitaja huduma zingine wanazokosa kuwa ni pamoja na kukosa taulo za kike, mafuta ya kupaka pamoja na kukosa fedha za kunyoa nywele
Credit:Nipashe
Social Plugin