Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa chama cha Ushirika Mahenge Amcos Julius Mbunda (kushoto) kuhusu mradi wa Shule unaojengwa na Chama hicho wengine pichani ni Afisa Ushirika pamoja na viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika MBIFACU, Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma hivi karibuni
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege (katikati) akipata maelezo kutoka kwa katibu wa chama cha Ushirika Kimuli Amcos Ernest Komba (kushoto) kuhusu mtambo wa kuchakata kahawa kulia ni Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma Bumi Masuba, Mbinga Mkoani Ruvuma
Mrajis Msaidizi wa Mkoa Bumi Masuba akieleza jambo wakati wa mafunzo elekezi ya Ushirika kwa Viongozi wapya wa Vyama vya Ushirika wa vinavyosimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika MBIFACU, mafunzo yaliyofanyika Mbinga Mkoani Ruvuma
Washiriki wa mafunzo elekezi ya Ushirika kwa Viongozi wapya wa Vyama vya Ushirika wa vinavyosimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika MBIFACU wakifuatilia mada na majadiliano ya mafunzo, Mbinga Mkoani Ruvuma.
Na.Mwaandishi Wetu,Mbinga, Ruvuma
Vyama vya Ushirika vimepewa wito wa kuendesha Miradi na mali za Vyama vya Ushirika kwa maslahi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika ili wanachama waweze kunufaika na miradi hiyo kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha umoja wa wanaushirika.
Wito huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege Mei 11, 2021 wakati alipotembelea miradi ya mbalimbali ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa cha Mbinga (MBIFACU) ikiwemo Mbicu hoteli, mashamba ya kahawa, pamoja na miradi ya shule na maghala ya vyama vya msingi vya MBIFACU wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma
Mrajis ameeleza kuwa ni muhimu wanachama kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na miradi inayoendeshwa na Vyama vyao vya Ushirika kuanzia ile miradi inayoendeshwa na Vyama vya msingi pamoja na vyama vikuu ili kuhakikisha wanachama wanakuwa na umiliki wa miradi hiyo pamoja na kupata faida zitokanazo na miradi hiyo.
“Ni lazima Vyama Vikuu na Vyama vya Msingi vyote vihakikishe kuwa vinaendesha na kuendeleza miradi hii kwa maslahi ya wanachama wake ili mwanachama anufaike na uwekezaji unaofanywa na chama chake na mwanachama awe ni sehemu ya mradi wa huo,” alisisitiza Mrajis
Akielezea umuhimu huo Mrajis alibainisha kuwa mwanachama anaweza kuwa na umiliki na miradi kupitia njia ya hisa za miradi ya hoteli, mashamba, viwanda zinazoweza kuuzwa na Vyama vya Ushirika kwa wanachama wake ambapo wanachama watakuwa wanapata gawio la faida zinazopatikana na miradi hivyo mwanachama kunufaika na miradi ya vyama.
Pamoja na kuangalia uwezekano wa faida za miradi kupunguza gharama za uendeshaji za vyama ili kutoa nafuu ya huduma kwa wanachama wake.
Akiongeza kuwa vyama viangalie hata katika miradi ya Shule vyama vinaweza kuweka viwango nafuu vya ada kwa watoto wa mwanachama.
Jambo ambalo litafanya Jamii kuwa sehemu ya mradi na pia kuvutia wengi zaidi kuwa wanaushirika.
Hivyo, amevitaka vyama vya Ushirika kwa kushirikiana na wadau kuongeza ubunifu huduma za Ushirika na kueleza Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Vyama katika hatua mbalimbali za kuboresha na kuimarisha huduma bora kwa wanachama wa Ushirika.
“Ili mwanachama wa Ushirika aweze kujivunia chama chake lazima kuwe na huduma za ziada anaweza kuzipata katika chama chake hii ni pamoja na masoko, pembejeo, bima za afya, pensheni kwa kufanya hivyo mwanachama atakuwa mlinzi wa kwanza wa mali na miradi ya chama,” alisema Mrajis
Pamoja na mambo mengine Mrajis amevitaka Vyama vya Ushirika kuwa na mipango ya uwekezaji inayotoa dira na kuelekeza shughuli za miradi ya maendeleo ya Vyama ya muda mfupi na muda mrefu ili kuhakikisha chama kinaendeshwa kwa utaratibu maalum uliopangwa na kuridhiwa na wanachama wake kupitia mikutano mikuu ya wanachama.
Katika hatua nyingine, Mrajis amewataka viongozi na wajumbe wa Bodi wapya wa Vyama vya msingi vya vinavyosimamiwa na Mbifacu waliokuwa wakipata mafunzo elekezi ya uendeshaji wa Vyama vya Ushirika yaliyokuwa yakiendeshwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhakikisha kuwa wanafikisha elimu ya ushirika kwa wanachama wao.
Akisisitiza lazima viongozi wa Ushirika kujiwekea mipango ya mafunzo kwa wanachama wanaporudi kwenye vyama vyao.
Mafunzo hayo yalihusisha wadau mbalimbali wanaoshirikiana kwa karibu na Sekta ya Ushirika ikiwemo Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mada zilizoelezwa kutolewa ni masuala ya misingi ya Ushirika, uandishi sahihi wa vitabu, uandaaji wa makisio, maadili na uadilifu katika uendeshaji wa Vyama.
Kwa upande wake mshiriki wa mafunzo hayo Winfrida Kapinga amesema mafunzo elekezi yanaenda kuongeza tija katika utendaji wao kama viongozi hasa kwa kuzingatia misingi ya Ushirika, uadilifu na maelekezo ya wataalamu ili kuepusha migogoro katika Vyama.
Akizungumzia katika vyama vya Ushirika, Winfrida ameeleza kuwa atatumia fursa hiyo kama kiongozi kwenda kuwaelimisha na kuhamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi zinazojitokeza katika vyama pamoja na shughuli za uzalishaji mali wa vyama vya ushirika ili kuondoa utegemezi na umasikini