Mwanamke mmoja kutoka kaunti ya Pokot Magharibi nchini Kenya amemtema mumewe kwa madai kwamba aliagizwa na Mungu kufunga ndoa na roho mtakatifu.
Elizabeth Nalem, mama wa watoto sita kutoka Makutano Town, alisema Mungu alimtokea wakati alikuwa amelala na kumuomba aachane na mumewe.
Tukio hilo lisilo la kawaida liliwashangaza wakazi wa Makutano ambao walikusanyika kushuhudia Bi harusi akijiandaa kuolewa na Roho Mtakatifu.
"Leo, mimi ni mmoja wa wale ambao wamepokea neno la Mungu. Nimepitia changamoto nyingi maishani na ikanibidi nitafute uso wa Mungu," aliwaambia waandishi wa habari.
Elzabeth aliingia kanisani akiwa amevalia gauni nyeupe kama pamba huku akifuatwa nyuma na marafiki zake wa karibu.
Ibada ilianza na mahubiri kutoka kwa mchungaji Albert Rumaita, ambaye alimuombea wakati akifungua ukurasa mpya wa maisha.
Baada ya sherehe hiyo, Nalem alisema alikuwa ameutumikia ulimwengu kwa miaka mingi, na sasa alikuwa mwanamke aliyebadilika tayari kwa kumtumikia Mungu wake.
Mma huyo wa watoto sita alisema mtumishi wa Mungu alimnunulia gauni, akamtafutia magari na kisha akaandaa sherehe hiyo iliyofanyika katika bustani ya Chelangaa.
Licha ya kwamba Nalem alidai alikuwa ameshauriana na mumewe, Joshua Nalem, alisema kuwa alishtuka kuhusiana na matukio ya siku hiyo akidai kwamba hakuwa na habari kuhusu hatua ya mkewe.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kila usiku mkewe alikuwa akiamka kuomba na alipomuuliza alinuna na kuhamia kwa jirani.
"Huyu ni mke wangu na nililipa mahari. Tuna watoto sita. Kifungua mimba wetu alimaliza kidato cha nne juzi," alidokeza.
Rumaita ambaye aliendesha sherehe hiyo alisema hakuwa na lingine ila kumfanyia mwanamke huyo alivyomuomba.
Chanzo - Tuko News
Social Plugin