Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inaboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia uwekezaji utakaoinua uchumi wa nchi na watu na mwongozo huo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuvutia uwekezaji na kuimarisha biashara.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana(Ijumaa, Mei 28, 2021) wakati akizindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa Bishop Rudin uliopo katika viwanja vya Mwembeni mjini Musoma. Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa mkoa huo wahakikishe watendaji, wataalamu na wananchi wanakuwa nyenzo ya kurahisisha kazi ya kuvutia uwekezaji.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hakikisha watendaji wote wa mkoa wanausoma na kuuelewa ipasavyo mwongozo huu. Hakikisha watendaji wako wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uaminifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa”.
Waziri Mkuu amesema mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji ambazo endapo zitatumika vema, zinaweza kuipaisha nchi kimaendeleo. “…Nitoe wito kwa uongozi mzima wa mkoa uhakikishe unaratibu vilivyo shughuli za uzalishaji hasa wa malighafi, bidhaa na huduma mbalimbali kwa ajili ya wananchi na mahitaji ya viwanda vya ndani.
Amesema miongoni mwa maeneo ambayo mkoa wa Mara unaweza kunufaika zaidi kwenye uwekezaji kutokana na fursa zilizopo ni kilimo, mifugo na uvuvi. Serikali ilitoa maelekezo yenye lengo la kuboresha sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ili kuzalisha malighafi za kutosha zitakazotumika kwenye viwanda.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Uwekezaji ishirikiane na mkoa ili kuwezesha Kituo cha Uwekezaji cha Kanda (TIC) kilichopo mkoani Mwanza kuanzisha Kituo cha Kutolea Huduma kwa Pamoja (One Stop Centre) ambacho kinapaswa kuwa na rasilimali za kutosha, vifaa na wataalam wote muhimu.
“Watu wote muhimu wanaopaswa kutoa huduma katika kituo wawepo, wakiwemo wataalamu wa Ardhi, Biashara, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Wakala wa Vipimo, NEMC, Bodi ya Nyama, Bodi ya Maziwa”.
Pia Waziri Mkuu ameziagiza idara zote za kisekta katika ngazi ya mikoa na wilaya, zishirikiane katika kubuni njia rahisi zitakazosaidia kuondoa urasimu na kurahisisha uwekezaji katika maeneo yao ili kuongeza ajira na vyanzo vya mapato ya Serikali.
“…Viongozi na watendaji wa sekta ya umma, fanyeni vikao na sekta binafsi kupitia Mabaraza ya Biashara ili kujadili na kutatua kero za kibiashara na uwekezaji zinazowakabili kwa wakati”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka mamlaka husika zihakikishe zinaweka mipango ya urasimishaji sekta isiyo rasmi, kurasimisha namba msimbo, kuwapatia wafanyabiashara ndogo ndogo maeneo ya kufanyia biashara na kuongeza kasi ya upimaji ardhi na kasi ya utekelezaji wa anuani za makazi na postikodi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuchochea fursa za kibiashara.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin