Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AMTEUA BRIGEDIA GENERALI NDUKU MABELE KUWA MKUU WA JKT, NA KANALI LYANGA SHAUSI KUWA MKURUGENZI WA SUMA - JKT


Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Brigedia Jenerali Rajabu Mabele

**

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan  tarehe 19 Mei 2021 amemteua Brigedia Jenerali Rajabu Nduku Mabele kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa. Hatua hiyo inafuatia kuteuliwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, Meja Jenerali Charles Mbugekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera hivi karibuni.

Brigedia Jenerali Mabele alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 25 Novemba 1993 na kutunukiwa Kamisheni kuwa Afisa tarehe 25 Machi 1995. Pamoja na taaluma nyingine za Kijeshi, Jenerali Mabele ana Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara (Master of Business Administration), alijikita katika Usimamizi wa Mashirika (Corporate Management).

Katika utumishi wake Brigedia Jenerali Mabele amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Afisa Usalama na Utambuzi katika Vikosi kadhaa; Afisa Mnadhimu Malipo na Afisa Malipo wa Kikosi Makao Makuu ya Jeshi; Mkurugenzi wa Fedha za Umma na Uhasibu (Director for Public Finance and Accounting) na baadae alihamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT), nafasi aliyohudumu hadi kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa.

Sambamba na uteuzi huo, Mhe. Rais amemteua pia Kanali Absolomon Lyanga Shausi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA-JKT. Kabla ya uteuzi huo Kanali Shausi alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo.

Kwa niaba ya Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo anawapongeza Brigedia Jenerali Mabele na Kanali Shausi kwa kuaminiwa katika nyaadhifa hizo na kuwatakia heri na fanaka katika utendaji wao.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com