Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema lengo la kukutana na wazee wa Dar es salaam kuwa ni pamoja na kwamba Dar es salaam ni mkoa uliokusanya watu wengi wa Tanzania hivyo akikutana na waliopo Dar es salaama wanawakilisha waliopo katika mikoa mingine.
Sababu ya pili ni kwamba umekuwa ni utamaduni kuwa tangu tupate uhuru,viongozi wa nchi wamekuwa wakiongea na wazee wakiwa na jambo lakini tatu amekuwa mlezi wa Mkoa wa Dar es salaam kupitia CCM.
"Mimi nimekuja hapa sina jambo bali nimekuja kuzungumza nanyi, niwasikilize, mnielekeze nikayafanyie kazi",amesema Rais Samia.
“Leo hii wazee wangu niwaombe radhi mahala hapa tulipo mtindo wa maisha umebadilika, tumekuja na viziba midomo, nyinyi pamoja na sisi na hii ni kwa sababu wazee ndio kundi ambalo lipo kwenye hatari sana kuambukizwa maradhi haya tulionayo na mkusanyiko huu ni mkubwa ili tuwakinge wazee wetu tumeamua leo tuvae barakoa,” amesema Rais Samia.
Idadi kubwa ya watu waliohudhuria mkutano wa Rais Samia na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam leo Ijumaa Mei 7, 2021 katika ukumbi wa Mlimani City wamevaa barakoa ambapo kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, imekuwa ikisisitizwa watu kuvaa barakoa kwa lengo la kujikinga na maradhi hao.
Social Plugin