RAIS SAMIA AWATAKA POLISI KUTOA ELIMU ZAIDI BADALA YA KUTUMIA SHERIA ZAO KUTOZA FAINI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Askari pamoja na Maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi pamoja na Wageni wengine Kurasini mkoani Dar es Salaam mara baada ya kufungua Kiwanda cha Ushonaji cha Jeshi la Polisi Tanzania.
***
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelitaka jeshi la polisi kujielekeza zaidi kutoa elimu badala ya kutumia sheria zao kutoza faini..

Rais Samia amesema hayo leo Mei 18, 2021 wakati akizindua kiwanda cha ushonaji cha jeshi la polisi kilichopo kilichopo katika Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam.

“Takwimu zinasema kuna upungufu wa makosa na upungufu wa makusanyo ya pesa kutokana na upungufu wa makosa, nataka nielekeze kwamba kazi ya Jeshi la Polisi ni kudhibiti makosa, tusijielekeze sana kwenye kipengele cha makosa na adhabu kwamba ni kitega uchumi, zaidi zitumike kudhibiti kuliko ukusanyaji wa faini na tozo nyingine. Nihimize suala la elimu kwa raia, naona vipindi vyenu kwenye TV lakini naomba muongeze zaidi.

Kuhusu hali ya usalama nchini, Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa hivi karibuni la kutaka kudhibitiwa kwa vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.


Hata hivyo, ametaka kudhibitiwa kwa wale wote wanaolijaribu Jeshi la Polisi kwa kuendeleza vitendo vya uhalifu.

“Baada ya kutoa ile kauli yangu kuhusu wahalifu IGP ulifanya mkutano na kuweka mikakati, lakini tunasikia bado kuna wanaojaribu kina cha maji, wanabonyeza bonyeza, nawaomba mjipange, wakibonyeza pasibonyezeke, kama mliweza huko nyuma hamuwezi kushindwa sasa. " Amesema

Rais Samia ameongeza kuwa kuanzia sasa miongoni mwa vigezo atakavyotumia katika kuwapandisha vyeo Makamanda wa polisi ni namna ambavyo wamekuwa wakikabiliana na vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.

“Hii sio kwa Dar es Salaam tu, bali nchi nzima, miongoni mwa vigezo tutakavyovitumia kuteua au kutengua Makamanda wa Polisi wa Mikoa ni kasi ya kudhibiti vitendo vya uhalifu, kwahiyo mkajitahidi kudhibiti vitendo vya ujambazi,” amesema Rais Samia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post