Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati akizungumza na viongozi mbalimbali wakati akikaribishwa na kukabidhiwa rasmi ofisi, leo mjini Shinyanga
Na Damian Masyenene, SHINYANGA
MKUU mpya wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati amepokelewa na kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack ambaye amehamishiwa mkoa wa Lindi, huku akiweka wazi nia yake ya kuimarisha ukusanyaji mapato, kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma na kuhimiza usikilizaji kero za wananchi na kufika maeneo ya miradi kujiridhisha na kinachotekelezwa.
Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika leo Mei 26, 2021 mjini Shinyanga katika ukumbi wa mkuu wa mkoa na kuhudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, mameya na wenyeviti wa halmashauri, wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, wawakilishi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, makundi maalum yakiwemo ya wenye ulemavu, wawkilishi taasisi binafsi na asasi za kiraia, viongozi wa taasisi za fedha, watendaji mbalimbali wa serikali, kamati za amani, kamati ya ulinzi na usalama na waandishi wa habari.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati amempongeza Zainab Telack kwa kazi kubwa aliyofanya na kuacha alama ya kukumbukwa ikiwemo kusimamia usalama, ukusanyaji mapato, usimamizi mzuri wa rasilimali, hivyo kumfanya kuwa kiongozi hodari na mchapa kazi.
Dk. Amesema kuwa anaufahamu mkoa wa Shinyanga kwani amewahi kufanya kazi mbalimbali akiwa na mashirika binafsi kwa mwaka mmoja, hivyo yuko imara na wala hatoyumbishwa na mtu yeyote, huku akiweka wazi kuwa ana misimamo ambayo imejikita kusimamia haki, ukweli na maslahi mapana ya wananchi walio wanyonge ili kujenga uchumi endelevu.
“Naifahamu Shinyanga ni nyumbani kuna baadhi ya vitu navifahamu kabla sijafika hapa, nimewahi kufanya kazi hapa. Ni muumini wa diplomsia na hoja jenzi zisizokinzana na imani za dini, muumini wa utawala bora, ukweli, ubunifu na ninapenda kazi kweli kweli. Watu wabunifu, wanaojituma na wanaopenda kazi kwangu ni marafiki,” amesisitiza.
RC Sengati ambaye alikuwa mhadhiri wa chou kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa miaka 10 kisha kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu kwa miezi 18 na Mkuu wa mkoa wa Tabora kwa miezi 10 kabla ya kuhamishiwa Shinyanga, ametaja vipaumbele vyake kuwa ni kuona mahusiano makubwa ya utajiri wa mkoa huo yakitafasiriwa kwa maisha bora ya wananchi wa Shinyanga, kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii.
“Kipaumbele namba moja nitaimarisha zaidi masuala ya usalama kwa kuhakikisha vitendo vinavyotishia usalama vinakomeshwa, namimi nitafuatilia kwa sababu ninataka usalama wa kweli ndani ya mkoa wa Shinyanga, ninataka watu wafanye kazi saa 24 bila hofu. Tunataka vibaka, wezi na majambazi waishe. Na yeyote atakayenikwamisha kwa hili ama zake ama zangu,” amefafanua.
Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni Mapato, ambapo atahakikisha mapato yanayopaswa kukusanywa yakusanywe ipasavyo, vyanzo vya mapato vitunzwe na kubuni vyanzo vipya na kila mmoja aonyeshe uadilifu, nidhamu na uzalendo, vilevile amesisitiza kuwa usimamizi matumizi ya fedha za umma nao ni kipaumbele chake huku akijipambanua kuwa yeye ni mpinga rushwa na wizi namba moja, hivyo anajiamini atasimamia jambo hilo ipasavyo.
“Nielekeze wakuu wa wilaya, jicho lenu nyoyo zenu ziwe kuzisimamia halmashauri katika masuala ya mapato na matumizi ili kusiwe na mianya ya rushwa, kashfa na hati chafu. Tushirikiane na tupendane tukitetea maslahi mapana ya wana Shinyanga na Tanzania, yeyote atakayejaribu kunigombanisha na watendaji wenzangu huyo atakuwa adui yangu namba moja.
“Kipaumbele kingine ni kuboresha huduma za jamii kwa kuboresha miundombinu, afya, elimu, maji na kusimamia upelekaji wa huduma za jamii. Hapa nielekeze watumishi tuwe tunatoka maofisini. Nitafuatilia hatua kwa hatua kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati, ubora na thamani ya fedha inaonekana. Kwa wanaofuatilia mimi ni mtu wa porini (field),” ameelekeza.
Katika hatua nyingine, Dk. Sengati amewataka watumishi na watendaji wa serikali mkoani humo kuhakikisha wanashughulikia kero za wananchi kwa kuwatembelea na kushughulikia shida zao na kujiridhisha na miradi inayotekelezwa.
“Niseme tu kwamba sitegemei kupata hati chafu katika mkoa wangu wakati wote nitakaokuwa hapa, ikitokea hivyo nitachukulia kwamba watumishi hawatoshi na taratibu za kiutendaji na kinidhamu zitachukuliwa kuhakikisha watendaji wazembe wanaoondoka,” amesisitiza RC Sengati.
Vilevile, Dk. Sengati katika kuhakikisha kuwa wanayaenzi na kuendeleza mazuri yaliyofanyika pamoja na kuleta maendeleo endelevu katika mkoa huo, amekuja na salamu mpya ya mkoa wa Shinyanga isemayo ‘Shinyanga, Kazi iendelee kwa maendeleo endelevu’, huku akiomba ushirikiano kwa wadau na makundi yote katika jamii kuhakikisha mkoa huo unaendelea kusonga mbele.
“Shinyanga ni mkoa wa kimkakati kiuchumi ndani ya taifa la Tanzania kwa sababu uko njia panda kuelekea mataifa ya jirani, mkoa unao rasilimali nyingi ikiwemo mifugo inayokadiriwa kufika milioni tano. Nitahakikisha naendelea kusimamia sifa hiyo ya mkoa wetu kuhakikisha tunaendelea kuchangia kwenye pato la taifa,” amesema.
Akizungumza wakati akimkaribisha mkuu mpya wa mkoa na kuwaaga watendaji wa mkoa huo, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amewashukuru wana Shinyanga kwa ushirikiano mkubwa waliompa akiwa kiongozi wao kwa miaka mitano na miezi mitatu, huku akikumbuka namna alivyofanikisha uwekaji wat aa za barabarani na uanzishaji wa viwanda Zaidi ya 700 katika mkoa huo.
Telack ameeleza kuwa wakati anafika Shinyanga alikuta mambo yakiwa magumu mkoa huo ukiwa umegubikwa na mauaji ya vikongwe, ramli chonganishi, mimba kwa wanafunzi na ndoa za utotoni, lakini sasa vimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa dini,ambapo amemuomba Mkuu mpya wa mkoa kuendeleza ushirikiano huo mkubwa na viongozi hao wa dini.
“Nilipofika hapa niliona mambo ni magumu (mambo fulani mengi), hatuwezi kuachia mkoa unaongozwa na wachawi wakati sisi tupo. Hivyo niliwakabidhi viongozi wa dini wametusaidia sana hata kumaliza mauaji ya Wazee na kutusaidia kufikisha ujumbe kwenye nyumba za ibada hasa masuala ya chanjo.
“Mkuu wa mkoa umekuja kwenye mkoa ambao uko salama, muhimu ni ushirikiano ili muweze kufika, kubwa kuliko mengine ni ushirikiano, hakuna siri ya mafanikio bila ushirikiano, nashukuru kwa ushirikiano mlionipa.
“Watu walidhani Shinyanga ni kisiwa na wengine walioona ni kama mkoa wa mateso, lakini tumeufungua kutoka kwenye boksi, watu wameufahamu na sasa watu wakihamishiwa hapa hawanung'uniki. Tumefanya kazi kubwa sana kuutangaza mkoa wetu,” ameeleza.
Kwa upande wake Mwenyekiti Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa amempongeza Zainab Telack kwa kazi kubwa aliyoifanya mkoani humo na kumtakia kheri, huku akimuomba kuyaendeleza yale mazuri katika kituo chake kipya cha kazi.
Mlolwa ameahidi kumpa ushirikiano wa kutosha Dk. Sengati ili kufanikisha mipango mizuri ya maendeleo, huku akimuomba kuongeza ubunifu mwingine kwenye kutekeleza miradi na mipango iliyopo kwenye ilani ya chama hicho
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga, Shekhe Khamis Balilusa, ameeleza kuwa wakati Telack anafika mkoani humo, kwa imani na tamaduni za wenyeji wa mkoa huo wa walimuweka kwenye matazamio kama ataweza kazi, lakini alidhihirisha namna gani alivyo kiongozi shupavu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wazee mkoani humo, Faustine Sengerema amemzungumzia Zainab Telack na kueleza kuwa ni kiongozi shirikishi kwa wakati wote aliwashirikisha wazee kwenye mambo mbalimbali ya maendeleo.
Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela (kushoto) akimkaribisha katika ofisi za mkoa huo, Mkuu mpya wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (kulia) baada ya kuwasili leo akitokea Tabora
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati akisalimiana na baadhi ya viongozi wa dini alipowasili leo katika ofisi za mkuu wa mkoa huo
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa (wa tatu kushoto)
RC Dk. Sengati akisalimiana na kuteta na baadhi ya watendaji wa ofisi ya mkoa wa Shinyanga alipowasili leo
Dk. Sengati akisalimiana na kuteta na baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri zilizopo katika mkoa huo, leo wakati wakimpokea
Afisa Rasilimali watu ofisi ya mkuu wa mkoa Shinyanga, Neema Rwegushora (kushoto) akimkabidhi ua kumkaribisha katika ofisi hizo, mkuu wa mkoa huo, Dk. Philemon Sengati
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akizungumza katika hafla hiyo
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) na Mkuu mpya wa mkoa huo, Dk. Philemon Sengati wakiomba wakati wa kufungua hafla hiyo ya makabidhiano
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ambaye alikuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga akizungumza katika hafla hiyo baada ya kukabidhi ofisi kwa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk.Philemon Sengati
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (wa pili kulia) akibadilishana hati ya makabidhiano na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack katika hafla ya kukabidhiana ofisi
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) akimpongeza mkuu wa mkoa huo, Dk. Philemon Sengati (kulia) baada ya kumkabidhi rasmi ofisi hiyo
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa akizungumza katika hafla hiyo
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya mkoa huo, Shekhe Khamis Balilusa akizungumza na kutoa neno la shukrani kwa niaba ya viongozi wa dini
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba (kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (kulia) wakati wa hafla ya kumkaribisha mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga
Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) mkoa wa Shinyanga, Richard Mpongo (wa pili kushoto) akimsalimia na kumpongeza Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati (wa tatu)
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo wakiwa kwenye hafla ya kumkaribisha mkuu wa mkoa
Baadhi ya wawakilishi wa taasisi binafsi na asasi za kiraia wakiwa kwenye hafla hiyo
Baadhi ya wawakilishi wa taasisi mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo
Washiriki wa hafla hiyo wakifuatilia makabidhiano hayo
Baadhi ya wawakilishi wa migodi, viwanda na TCCIA wakiwa ni sehemu ya hafla hiyo
Hafla ikiendelea
Baadhi ya wawakilishi wa taasisi za fedha wakiwa ni sehemu ya hafla hiyo
Hafla ikiendelea
Baadhi ya wawakilishi wa vyama vya siasa wakiwa ni sehemu ya hafla hiyo
Wawakilishi wa makundi maalum wakifuatilia hafla hiyo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba akiteta jambo na baadhi ya wawakilishi wa taasisi za kifedha mkoani humo
Picha ya pamoja na wakuu wa wilaya
Picha ya pamoja na viongozi wa dini
Picha ya pamoja na wawakilishi wa taasisi zisizo za kiserikali
Picha ya pamoja na viongozi wa CCM
Picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama
Picha ya pamoja na wawakilishi wa taasisi za fedha
Picha ya pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa
Picha ya pamoja na wawakilishi wa makundi maalum na wajasiriamali
Picha zote na Shinyanga Press Club Blog