Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YASISITIZA UPATIKANAJI WA TAARIFA SAHIHI ZA UVUVI MDOGO

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesisitiza upatikanaji wa taarifa sahihi za uvuvi mdogo nchini kwa kuangaza taarifa za wavuvi wadogo zilizofichika ili ziweze kutumika kwa mipango ya maendeleo endelevu kwa lengo la kukuza Uchumi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa warsha ya wadau wa sekta ya uvuvi ya kupitia matokeo ya utafiti wa mchango wa Uvuvi mdogo iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (DRTE) Dkt. Erastus Mosha mjini Morogoro (21.5.2021).

Akisoma hotuba hiyo, Mkurugenzi amewakumbusha wadau kuwa Uvuvi ni sayansi, hivyo usimamizi wa rasilimali hiyo ni muhimu na unahitaji taarifa za kutosha za kitafiti ili kufikia malengo ya kuwa na Uvuvi endelevu nchini.

Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya Uvuvi kwa muda mrefu kuwa ni kukosekana kwa taarifa sahihi za mavuvi, zana haramu, idadi ya wavuvi, vyombo vya Uvuvi na nyinginezo.

Pia alisema ana matumaini makubwa kuwa matokeo ya utafiti huo wa kuangaza taarifa za uvuvi zilizofichika yatasaidia kuboresha mipango ya sekta ya Uvuvi nchini kuendana na kasi ya maendeleo ya viwanda na kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la Taifa kutoka asilimia 1.7 hadi asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025.

Aidha katika hotuba yake mgeni rasmi aliwafahamisha wadau kuwa,mwaka 2016 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliingia makubaliano na Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) ili kutekeleza mradi wa kuwezesha utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo unakuwa Endelevu katika Muktadha wa Uhakika wa Chakula na Kuondoa umasikini.

Aliongeza kuwa matokeo mazuri yanayoendelea kutokea yanatokana na Mradi wa kutekeleza Mwongozo wa Wavuvi Wadogo (SSF Guidelines),ambapo Wizara kwa mara nyingine tena ilisaini makubaliano ya kutekeleza Mradi huo wa kuimarisha mchango wa Uvuvi Mdogo kwa usalama wa Chakula na Maisha Endelevu.

Kwa upande wake kiongozi wa timu ya utafiti Dkt. Paul Onyango kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam anasema utafiti huo uliofadhiliwa na FAO ulianza Mwaka 2018, na umefanyika kwenye takribani nchi 40 Duniani.

Akigusia matokeo ya utafiti huo, Dkt. Onyango anasema kuwa kuna taarifa nyingi zilizofichika ambazo zinasababisha thamani ya mchango wa uvuvi mdogo kiuchumi kuonekana ndogo sana tofauti na uhalisia wenyewe.

Dkt. Onyango anabainisha mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hiyo kuwa ni vyema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) kuwa na bajeti maalum ya ukusanyaji takwimu za wavuvi wadogo, kuongeza wakusanya takwimu wenye weledi wa kazi hiyo na pia kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa sahihi kwa Serikali.

Mvuvi mdogo Bw. Peter Sumuni kutoka ziwa Nyasa akizungumzia sababu ya wao wavuvi kutokutoa takwimu sahihi kwa maafisa Uvuvi wa maeneo yao, anasema kuwa hawana elimu ya kutosha ya umuhimu wa takwimu hizo pia ushirikiano wao na maafisa Uvuvi hauridhishi.

Aidha Bi.Sijali Hemedi kutoka Kilwa ambaye ni mkusanya takwimu ameelezea kuwa changamoto ni uchache wa wakusanyaji wa takwimu pamoja na uwezeshwaji wa rasilimali Fedha kwa ajili ya kazi hiyo.

Ili kufanikisha lengo la kuwa na Uvuvi Endelevu kwa ajili ya kukuza uchumi, Bw. Yusuph Semuguruka kutoka ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anasisitiza ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na TAMISEMI ikiwa ni pamoja na kufuata taratibu za kupeana taarifa katika utekelezaji wa shighuli mbalimbali za sekta ya Uvuvi nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com