SGR KUTUMIA MIFUMO YA KISASA KUZUIA AJALI ZA TRENI
الأحد, مايو 23, 2021
IMEELEZWA kuwa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), unatarajiwa kuwekwa mifumo ya kisasa ambayo itasaidia kuzuia ajali ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa uendeshaji wa reli hiyo na ambao hautamruhusu dereva kuzidi ama kupunguza mwendo uliowekwa.
Hayo yamesemwa na Meneja Msaidizi wa mradi wa reli ya Kisasa, kipande cha Morogoro - Makutopora (Km 422) kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Christopher Mang’wela, wakati akizungumza na wahandisi kutoka Serikalini na Sekta Binafsi ambao wametembelea mradi huo uliofika asilimia 61, jijini Dodoma, kwa ajili ya kujifunza utekelezaji wa mradi kuanzia hatua mbalimbali zilizotekelezwa.
“Kama mnavyoona, mradi umefika asilimia 61, na uendeshaji wake utakuwa ni wa kisasa kwani utawekwa vifaa maalum vya kumuongoza dereva wa treni ili kuzuia ajali.” amesema Mhandisi Mang'wela.
Awali, akizungumza kwa niaba ya wahandisi hao, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, ameeleza kuwa anaona nia ipo na uwezo kwa watanzania katika kusimamia miradi mikubwa inayoendelea nchini huku tukiwa na usimamizi mdogo kutoka wenzetu wa nje na hivyo kuwaleta wahandisi wetu katika mradi kutaongeza chachu ya kuchukua zabuni nyingi za miradi mikubwa inayoatarajiwa kuanza na kuendelea hapa nchini.
"Tumetembelea mradi huu katika baadhi ya maeneo ambapo tumeridhishwa na mradi huu na tumeona unaendeshwa vizuri kuanzia mwanzoni hadi hapa ulipofika kwani kupitia mradi huu wahandisi wamejifunza mengi", amefafanua Mhandisi Barozi.
Aidha, Mhandisi Barozi ameongeza kuwa kupitia vipande vitatu vya utekelezaji wa mradi huo, wahandisi wa hapa nchini wamepata utaaalamu wa kutosha na hivyo kuweza kuisaidia Serikali kwa utekelezaji wa awamu zinazofuata endapo watawezeshwa katika suala zima la upatikanaji wa vifaa.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhandisi, Dkt. Ramadhan Mlinga, amesema kuwa wahandisi waliopo kwenye mradi huo kufuatilia kwa makini kipindi cha mwisho cha utekelezaji wa mradi huo kwani kipindi hiki husaidia kuboresha utekelezaji wa miradi inayofuata kwa kuangalia changamoto zilizowakabili katika utekelezaji wa mradi uliopita na kutafutia ufumbuzi katika utekelezaji wa mradi ujao.
"Kwa kawaida miradi ina hatua tano za utekelezaji ikiwemo kuibua mradi, kupanga jinsi ya kutekeleza mradi, utekelezaji wa mradi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi na kufunga mradi ambapo hivi ni lazima vizingatiwe ili mradi ufanikiwe”, amesisitiza Mlinga.
Naye, Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Nyandalo Hezron, amesema kuwa wamefurahishwa na mafunzo hayo kwani yamewasaidia kujua uhalisia wa yale waliyojifunza darasani na kuyaleta katika utekelezaji ambayo yawakumbusha miongozo mbalimbali katika usimiamizi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayoendelea.
Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ulioanza mwezi Aprili 2017 wenye lengo la kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji nchini na nchi za jirani unaendelea kutekelezwa ambapo hivi karibuni kazi za ujenzi sehemu ya Isaka – Mwanza yenye urefu wa kilometa 341 unatarajiwa kuanza.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin