MSIMU WA UNUNUZI WA PAMBA KITAIFA 2021/2022 WAZINDULIWA
Wednesday, May 12, 2021
Msimu wa ununuzi wa Pamba kitaifa 2021/2022 umezinduliwa wilayani Busega, mkoani simiyu. Akizindua, msimu wa ununuzi wa pamba, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Mwera amesema ushirikiano wa wadau wa kilimo cha pamba utaongeza tija ya zao hilo.
“Zao la pamba ni miongoni mwa mazao ya kimkakati, hivyo wadau washirikiane ili kuongeza tija”, alisema Mhe. Mwera. Katika kuleta tija ni vyema wakulima kufuata kanuni za kilimo bora ikiwemo upandaji wa pamba kwa nafasi inayotakiwa ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo, aliongeza Mhe. Mwera.
Awali, Mkurugenzi wa bodi ya pamba, Bw. Marko Mtunga amesema uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba una manufaa makubwa hivyo Busega imepewa heshima kubwa, na hii imetokana na kazi kubwa ya usimamizi mzuri wa viongozi wa Wilaya katika kilimo cha pamba. “Katika msimu wa 2020/2021, wilaya ya Busega imezalisha takribani kilo milioni 3, lakini msimu wa mwaka 2021/2022 tunategemea uzalishaji zaidi ya kilo milioni 10” aliongeza, Mtunga.
Aidha, Mhe. Mwera amesema licha ya Wilaya kuwa na uzalishaji mzuri katika zao la pamba, lakini changamoto kubwa inayowakabili wakulima, ikiwemo wadudu. Hali hiyo imewafanya wakulima wengi kushindwa kutambua jinsi ya kukabiliana na wadudu wanaoshambulia zao la pamba, hivyo bodi ya pamba itoa elimu zaidi kwa wakulima ikiwemo elimu ya kupambana na wadudu.
Kauli mbiu ya uzinduzi wa msimu ununuzi wa pamba kitaifa 2021/2022 inasema “Tuboreshe Ubora na Usafi wa Pamba kwa Uhakika wa Soko na Malipo kwa Wakati”. Kauli ambayo imeelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima wa zao la pamba. Wanunuzi wa pamba walioshiriki uzinduzi huo wamesema wapo tayari kununua pamba na kuahidi wakulima watalipwa kwa wakati. Katika uzinduzi huo, Serikali imetoa bei elekezi ya zao la pamba kwa msimu wa 2021/2022, ambapo pamba daraja A itanunuliwa kwa Tzs 1,050 na daraja B itanunuliwa kwa Tzs 525.
Baadhi ya wa wakulima wa pamba Wilayani Busega wanasema Serikali, wakulima na wadau wengine wanapaswa kushirikiana ili kuongeza uzalishaji wa zao la pamba nchini. Kwa upande mwingine wameiomba Serikali kutoa elimu zaidi ya zao hilo ikiwemo kanuni bora za ulimaji wa zao hilo.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin