Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akionesha vifaa vya kupigia ramli chonganishi (Picha kutoka maktaba ya Malunde 1 blog)
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia mwanaume aliyejulikana kwa jina la Ally Mbwan Libuye (50) kwa kosa la kupiga ramli chonganishi akidai anafichua mtu mchawi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mjini Kahama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema mtuhumiwa huyo alifika Wilayani Kahama Mwezi Mei , 2021 akiwa ametokea Mkoa wa Pwani- Rufiji.
"Alikuja Kahama kwa ajili ya kufanya shughuli za kubaini wachawi (KAMCHAPE) kwenye kijiji cha Zongomela na vijiji jirani hapa Wilayani Kahama, ambapo mtuhumiwa huyu amekuwa akipita mitaani akiwa ameambatana na watu na kubaini baadhi ya nyumba ambazo zina wachawi kitendo ambacho ni sawa na kupiga ramli chonganishi/kumtaja mtu mchawi".
Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wananchi Mkoa wa Shinyanga kuachana na vitendo vya kuwataja wachawi kwani hupelekea kutokea kwa mauaji.