Watu wawili waliotoka gerezani Aprili 12, 2021 kwa msamaha wa Rais wameuawa baada ya kukamatwa wakidaiwa kuiba vitu mbalimbali huko kwa Mathiasi mjini, Kibaha mkoani Pwani.
Wawili hao walifungwa kwa makosa ya wizi katika kesi ya jinai namba 273/2020 na 260/2020 katika gereza la Mkuza mjini Kibaha.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Wankyo Nyigesa, amesema jana Mei 10, 2021 watu hao wameuawa Mei 8 alfajiri kwa kupigwa na mawe, mapanga na fimbo na wananchi wenye hasira waliowatuhumu kuhusika kwenye tukio la wizi.
"Hawa watu wametambuliwa ni Ramadhani Mohamed maarufu kwa jina la Seven au Ali (28) mkazi wa kwa Mathiasi na Idd Hamisi maarufu Chuga (30) mkazi wa mtaa Jamaika, wote walikuwa wamerudi uraiani hivi karibuni kwa msamaha wa Rais," amesema Nyigesa.
Hata hivyo, Kamanda Nyigesa ameshauri wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha hasira na badala yake watoe taarifa polisi inapotokea tukio la wizi kwenye maeneo yao, ili watuhumiwa wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Social Plugin