WANAVIJIJI 30 SIMIYU WAPEWA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA TEMBO


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Pellage Kauzeni akizungumza na madiwani wa Wilaya ya Meatu kuhusu mikakati ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya kukabiliana na tembo wanaovamia makazi ya watu katika kikao kilichofanyika Wilayani Meatu mwishoni mwa wiki.
Wananchi waliopewa mafunzo ya kukabiliana na tembo wakionyesha kwa vitendo namna ya kutumia honi ili kumfukuza tembo aliyevamia makazi ya watu katika onesho lililofanyika baada kikao cha Wizara ya Maliasili na Utalii na Madiwani wa Wilaya Meatu kilichofanyika mwishoni mwa wiki.
Wananchi waliopewa mafunzo ya kukabiliana na tembo wakionyesha kwa vitendo namna ya kutumia wigo wa pilipili na oili chafu ili kumfukuza tembo aliyevamia makazi ya watu katika onesho lililofanyika baada kikao cha Wizara ya Maliasili na Utalii na Madiwani wa Wilaya Meatu kilichofanyika mwishoni mwa wiki.

*******************************

Na Happiness Shayo- MEATU

Wanavijiji 30 kutoka wilaya zote za mkoa wa Simiyu wamefundishwa namna ya kukabiliana na wanyama waharibifu hasa tembo ikiwa ni mwendelezo wa mikakati ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuhakikisha usalama wa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye changamoto ya kuvamiwa na tembo.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Pellage Kauzeni alipofanya kikao na madiwani wa Wilaya ya Meatu mwishoni mwa wiki.

Bw. Kauzeni amefafanua kuwa mafunzo hayo yamefanyika chini ya Mradi wa utafiti wa tembo kwa ukanda wa Serengeti, Maswa na Ngorongoro.

Ametaja mafunzo yaliyotolewa kwa wananchi hao kuwa ni kutumia honi, kutumia mabomu ya pilipili na kutumia mabomu ya kisasa ya kufukuza tembo.

Njia nyingine zilizofundishwa za kupambana na tembo ni kutumia wigo wa pilipili na oili chafu pamoja na kutengeneza tofali au mkate wa pilipili na kinyesi cha wanyama kama ngombe,mbuzi n.k.

Bw. Kauzeni ameweka bayana kuwa njia hizo za kupambana na wanyama waharibifu zimeshawahi kutumika katika maeneo mbalimbali na zimeleta matokeo chanya.

“Njia hizi zimeshawahi kutumika na Jumuiya za Hifadhi kwa Jamii (WMA) za Kaskazini mwa Tanzania kupitia mradi wa Fredkin na pia Kusini mwa Tanzania upande wa Selous Game Reserve na zimeonyesha mafanikio makubwa” amefafanua Bw. Kauzeni.

Akizungumzia mikakati ya Serikali ya kuendelea kupambana na wanyama waharibifu Bw. Kauzeni amesema Serikali kupitia taasisi ya Tanzania Wildlife Research Institute (TAWIRI) inaendelea na tafiti ili kugundua mbinu za gharama nafuu zaidi zitakazotumiwa na wananchi kupambana na tembo na pia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuelimisha wananchi ili kupunguza changamoto ya uvamizi wa wanyama waharibifu katika makazi ya watu.

Naye, Mkazi wa Kijiji cha Mwanzalamba Wilaya ya Meatu, Sololo Malando amesema kuwa amefundishwa mbinu mbalimbali za kujilinda na wanyama waharibifu kama kutumia vilipuzi vya kurusha kwa mkono.

“Mbinu hii ya kutumia vilipuzi ikitumika vizuri itasaidia sana wananchi kuondokana na hili tatizo la tembo kwa kuwa inasaidia kuwakimbiza tembo endapo wamevamia mashamba” amesema Malando.

Mkazi mwingine wa wilaya ya Meatu, Magembe Sita ametaja mafunzo aliyoyapata akitolea mfano wa mafunzo ya kutumia tochi, honi na baruti ya kutumia mchanga na pilipili kufukuza tembo.

Kikao hicho kiliambatana na maonyesho ya mbinu za kukabiliana na tembo yaliyofanywa na wanavijiji kutoka wilaya za Mkoa wa Simiyu na kushuhudiwa na wakuu wa wilaya za Busega, Itilima na Meatu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post