Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

YWCA YAONYA WAZAZI KUTUMIA FURSA MIMBA ZA UTOTONI KUJIPATIA MALI

 

Katibu wa Shirika la Young Women's Association (YWCA) mkoani Shinyanga, Marysiana Makundi ambalo linatekeleza mradi wa kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga , akizungumza kwenye kikao na wajumbe wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kwenye kata hiyo.

Na Marco Maduhu, Shinyanga.

WAZAZI mkoani Shinyanga, wameonywa tabia ya kutumia fursa mimba za utotoni kwa kumaliza kesi kimya kimya na upande wa mtuhumiwa, kwa kupewa pesa ama mifugo, na kusababisha wahalifu kutofungwa jela, hali ambayo inachochea vitendo hivyo kuendelea ndani ya jamii mkoani humo na kuzima ndoto za wananafunzi wa kike.

Katibu wa Shirika la YWCA Marysiana Makundi, ambao wanatekeleza mradi wa kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, amebainisha hayo leo kwenye kikao chao na wajumbe wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ndani ya Kata hiyo.

Alisema baadhi ya wazazi mkoani humo wamekuwa kikwazo kikubwa cha kumaliza tatizo la mimba za utotoni, kutokana na kugeuza mimba hizo kama fursa za kujipatia mali, ambapo kesi inapokuwa ikiendelea mahakamani wao huenda kumaliza na upande wa mtuhumiwa, kwa kupewa pesa ama mifugo na kisha kuacha kuhudhulia mahakamani kutoa ushahidi na kesi kufutwa.

“Mimi nilishakutana na kitu kama hiki kuna kesi moja nilikuwa naishughulikia ya mwanafunzi kupewa ujauzito, lakini cha ajabu wazazi wa huyo binti wakakutana na upande wa mtuhumiwa wakamailizana kwa kupeana fedha huku mimi nikiwa sijui, mara nikaanza kukosa ushirikiano kutoka kwao hadi kesi ikafutwa, na mtuhumiwa akaachiwa huru,”alisema Makundi.

“Niwaambie tu wazazi mkoani Shinyanga tuache hii tabia ya kugeuza fursa mimba hizi za utotoni kwa malengo ya kujipatia pesa ama mifugo, wanaoumia ni watoto sababu wanazima ndoto zao na kuingia kwenye majukumu ya kiutu uzima ambayo hawayawezi, hivyo naomba tuungane kwa pamoja kutokomeza huu ukatili dhidi ya watoto,”aliongeza.

Katika hatua nyingine aliwataka wazazi mkoani humo kuacha kuendekeza mila na desturi kandamizi ambazo zilishapitwa na wakati, ambazo ndio zimekuwa chanzo cha kuendelea kuwepo kwa matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.

Naye Ofisa Maendeleo ya jamii kata ya Ibadakuli Mwijage Patrick, aliwataka wazazi kujenga utamaduni pia wa kuzungumza na watoto wao juu ya makuzi yao pamoja na kuwapatia elimu ya afya ya uzazi, sambamba na kufuatilia mienendo yao ili kuwaepusha dhidi ya matukio ya ukatili.

Kwa upande wake Polisi Kata wa Ibadakuli Emmanuel Maganjila, aliwataka watoto mkoani Shinyanga wapaze sauti dhidi ya matukio ya ukatili, kwa kutoa taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria, huku akiwataka wadau waendelea kutoa elimu ya ukatili kwa wananchi na kuwaeleza madhara yake.

Nao waelimishaji wa masuala ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii Mary John, alisema jamii inapaswa kubadilika na kuwaona watoto wa kike wapo sawa na wakiume, na kuacha kuwafanyia matukio ya ukatili ambayo huharibu ndoto zao pamoja na wengine kuathirika kisaikolojia.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Katibu wa Shirika la YWCA Marysiana Makundi akizungumza kwenye kikao hicho.
Afisa miradi wa Shirika la YWCA John Eddy akiongoza mjadala kwenye kikao hicho.
Mtendaji wa Ibdakuli Sara Wamkuru akizungumza kwenye kikao hicho.
Afisa maendeleo ya jamii Kata ya Ibadakuli Mwijage Patric akizungumza kwenye kikao hicho.
Polisi Kata ya Ibadakuli Emmanuel Maganjila, akizungumza kwenye kikao hicho
Wajumbe wakiwa kwenye kikao.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao.

Na Marco Maduhu- Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com