Na. Edward Kondela
Serikali imepanga kuweka utaratibu wa kutambua hatua mbalimbali za upatikanaji wa nyavu za uvuvi tangu kutengenezwa kwake hadi kusambazwa na kumfikia mvuvi ili kudhibiti usambaaji wa nyavu zisizohitajika kisheria hapa nchini.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha hayo jana (22.05.2021) wakati akizungumza na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kanyala kilichopo Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo na kubainisha kuwa serikali inataka suala la kuchoma nyavu lipungue au liishe kabisa.
“Tumejipanga vyema sana wavuvi mmekuwa mkipata sintofahamu kubwa unaenda dukani kununua nyavu ya milimita nane (8) ukija nayo huku ikipimwa inaonekana iko chini ya milimita hizo ambapo ni kinyume na sheria na wewe kuchukuliwa hatua, sasa tutapambana na wauzaji na wasambazaji wa nyavu hizo.” Amesema Mhe. Ulega
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha nyavu za uvuvi zinakuwa katika viwango vinavyotambulika, wizara itaweka pia utaratibu wa kuwepo kipimo kimoja ambacho kitatambulika nchi nzima kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kumuokoa mvuvi asiendelee kuumizwa kwa kuarifiwa kuwa nyavu zake ziko kinyume na sheria.
Naibu waziri huyo amewapongeza pia wakazi wa Kijiji cha Kanyala kwa kuonesha uelewa mpana juu ya kutotumia zana haramu kwa kushirikiana na serikali jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limepunguza shughuli za uvuvi zisizozingatia sheria za nchi.
Kuhusu kuanzishwa kwa vyama vya ushirika vya wavuvi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kuwawezesha wavuvi kupitia vyama hivyo kwa kupata mikopo ili waweze kununua vyombo vya kisasa zaidi vya shughuli za uvuvi.
“Vikundi vya ushirika vinafanya vizuri sana na wengine wamejitengenezea vyombo vya uvuvi, tuweke utaratibu mzuri tusirudi nyuma nimekuja kutazama namna mnavyosonga mbele nataka kurudisha ari ya kufanya vizuri sana, nataka nirudi tena hapa kukabidhi hundi.” Amefafanua Mhe. Ulega
Katika kuhakikisha vyama vya ushirika vya wavuvi vinanufaika na mikopo kupitia taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Naibu Waziri Ulega amevitaka vyama ambavyo tayari vimepatiwa mikopo kufanya marejesho kwa wakati ili viweze kuwa na sifa ya kukopeshwa tena pamoja na kuwezesha vyama vingine kupata mikopo na kukuza sekta ya uvuvi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe. Eric Shigongo akizungumza katika mkutano huo ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi namna inavyohakikisha inasimamia maslahi ya wavuvi na kuiomba kuhakikisha inadhibiti nyavu za uvuvi zisizotakiwa kisheria kabla hazijafika kwa wavuvi, kwa kukagua nyavu kwa watu au makampuni yaliyopewa vibali vya kuingiza nyavu hizo nchini.
Aidha, amesema serikali haiko tayari kukandamiza raia wake wakiwemo wavuvi na kukemea vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wakati wa ukaguzi wa nyavu za uvuvi kwa wavuvi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Emmanuel Kipole amekemea pia vitendo vya rushwa na kuwataka wavuvi wasikubali kutoa rushwa kwa mtendaji yeyote wa serikali kwani kwa kufanya hivyo wanakuwa wanahalalisha kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo.
Amewataka watendaji wanaohusika na ukamataji wa zana za uvuvi zisizotakiwa kisheria kufuata sheria za nchi kwa kuwa vitendo vya rushwa vinabomoa nchi na kusababisha kutokuwepo kwa mahusiano mazuri baina ya watendaji hao na wavuvi.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kanyala wakizungumza katika mkutano wa Naibu Waziri Ulega, wamelalamikia baadhi ya vyama vya ushirika vya wavuvi kukosa mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha licha ya kufuata taratibu ambazo zimekuwa zikianishwa na taasisi hizo, jambo ambalo Mhe. Ulega alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw. Japhet Justine katika mkutano huo juu ya jambo hilo ambapo mkurugenzi huyo aliahidi kulifanyia kazi.
Wakazi hao pia wameiomba serikali kutokomeza kabisa uwepo wa nyavu haramu ili waweze kununua nyavu zinazotakiwa kisheria kwa kuwa wamekuwa wakipata hasara kwa kununua nyavu zisizotakiwa kisheria bila kufahamu na hatimaye kukamatwa kwa nyavu hizo na kuchomwa moto jambo ambalo limekuwa likiwarudisha nyuma kimaendeleo.
Akiwa katika Wilaya ya Sengerema, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiambatana na Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe. Eric Shigongo na mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Emmanuel Kipole pamoja na viongozi wengine, amefika katika Kijiji cha Zilagula na kukutana na Chama cha Ushirika wa Wavuvi Zilagula na kujionea namna mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 waliopatiwa na TADB wanavyoutumia kwa kutengeneza boti za uvuvi, vichanja vya kuanikia dagaa, kujenga eneo la kuhifadhia samaki pamoja na kujulishwa mikakati mbalimbali ambayo chama hicho kitaendelea kufanya kupitia fedha hizo.
Akiongea na wakazi wa Kijiji cha Zilagula Mhe. Ulega amekitaka Chama cha Ushirika wa Wavuvi Zilagula kuwasaidia vijana na kutaka wataalam kufikishwa katika kijiji hicho ili kutoa elimu ya matumizi bora ya fedha za mikopo ili mkopo huo uweze kuwa na tija zaidi kwao na jamii inayowazunguka.
Amekitaka chama hicho kufanya kazi vizuri zaidi ili siku zijazo waweze kununua boti za kisasa zaidi za uvuvi na kuwataka wakazi wa Kijiji cha Zilagula kuunga mkono uwepo wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Zilagula.
Ameongeza kuwa kupitia chama hicho wavuvi wataweza kuuza samaki kwa bei nzuri zaidi badala ya kulanguliwa na watu wachache ambao wamekuwa wakinunua samaki kwa bei ndogo zaidi na wenyewe kwenda kuuza kwa bei kubwa katika masoko mengine.
Social Plugin