Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Wakandarasi kutoka Kampuni 34 ambao wanatekeleza Mradi wa usambazaji umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili (hawapo pichani) kilichofanyika leo Mei 25,2021 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza wakati wa kikao na Wakandarasi kutoka Kampuni 34 ambao wanatekeleza Mradi wa usambazaji umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili (hawapo pichani) kilichofanyika leo Mei 25,2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini REA, Mhandisi Amos Maganga akizungumzawakati wa kikao cha Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani na Wakandarasi kutoka Kampuni 34 ambao wanatekeleza Mradi wa usambazaji umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili (hawapo pichani) kilichofanyika leo Mei 25,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya Wasimamizi wa Miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka Wizara ya Nishati, watendaji wa REA, TANESCO na wakandarasi wa mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (hayupo pichani) kilichofanyika leo Mei 25,2021 jijini Dodoma.wa mwisho kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu.
Baadhi ya Mameneja wa TANESCO kutoka sehemu mbalimbali nchini pamoja na Wakandarasi wa mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati alipofanya kikao na wakandarasi hao jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaagiza wakandarasi walioshinda zabuni ya kutekeleza Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili kuripoti kwa viongozi wa wilaya ambako wanatekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini pamoja na kuanza utekelezaji wa Mradi huo mara moja.
Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo leo Mei 25,2021 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi kati ya Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), TANESCO na wakandarasi amesema kuwa Kuna faida nyingi za kuripoti katika ofisi za wilaya na vijiji ikiwa ni pamoja na kupata uhakika wa usalama wa rasilimali watu na vifaa vya mradi. Madhara ya kutoripoti ni makubwa zaidi”
“Baada ya mkutano huu msambae katika maeneo yenu ya kazi mara moja..niwaombe sana muende site muanze kuchapa kazi” alisema na kuwataka wahakikishe wanaunganisha umeme kwenye vijiji vyote nchini ambavyo havina huduma ya umeme ndani ya miezi 18 kuanzia sasa.
Amesema kuwa wakandarasi watekeleze miradi kwa kushirikisha viongozi na wananchi ili kujenga mahusiano mazuri na watoe kipaumbele kwa kutoa ajira hasa kazi za vibarua kwa vijana wa vijijini ambako miradi ya kusambaza umeme inatekelezwa.Dkt. Kalemani amewataka wakandarasi kuwaunganishia umeme wananchi ndani ya siku 14 baada ya kufanya malipo ya kuunganishiwa umeme na wasibague nyumba za tembe, vibanda vya biashara pamoja na maeneo ya mazizi ya mifugo kwa wananchi watakaohitaji huduma hiyo.
Aidha Dkt.Kalemani ametoa onyo kwa wakandarasi na mafundi wanaoweka mifumo ya nyaya ndani ya nyumba ‘wiring’ ambao sio waaminifu kuacha tabia hiyo mara moja ya kuwatapeli wananchi na kuwataka REA na TANESCO kuhakikisha kero hiyo haitokei tena katika miradi ya kusambaza umeme vijijini.Miongoni mwa mambo ambayo Waziri amewasisitizia wakandarasi kuyazingatia ni pamoja na kununua vifaa bora vinavyotengenezwa na viwanda vya ndani ya nchi na amewataka wenye viwanda kutengeneza vifaa vyenye ubora na kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya miradi ya kusambaza umeme vijijini.
Amesema kutokana na mradi huo kutohusisha ulipaji fidia kwa wananchi ambao sehemu ya maeneo yao itatumika kupitishia miundombinu ya umeme, wakandarasi wanapaswa kutumia busara wakati wa ujenzi wa miundombinu hiyo. “Mwananchi ana kiwanja chake kidogo, lakini nguzo inatakiwa kuwekwa katika eneo hilo.
Utakuta badala ya nguzo kuwekwa mahali ambapo ataweza kuendelea na shughuli nyingine katika eneo hilo, mkandarasi anasimika nguzo katikati ya eneo…naomba mkatumie busara mkapitishe miundombinu ya umeme pasipo kuathiri matumizi eneo la mwananchi,” amefafanua.
Hata hivyo, Dkt. Kalemani amesema ili kupunguza hujuma za vifaa na miundombinu, wakandarasi wanapaswa kuajiri vibarua ambao ni waaminifu na wawe wa kwanza kulinda vifaa vyao na aliwataka wananchi kuacha kuhujumu miundombinu ya kusambaza umeme vijijini.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato ameahidi kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati huku akiwataka wasimamizi wa mradi kuwa vikao kazi na wakandarasi katika maeneo ya miradi na kuandaa ripoti za vikao hivyo ambazo zitatumika kwa ajili ya maelekezo ikiwa ni pamoja na kuboresha utekelezaji wa Mradi.
"Tutajikita zaidi kusimamia mikataba yenu, kuna wengine hamzingatii masharti ya mikataba yenu lazima tukumbushane” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga amewahakikishia wakandarasi kuwa Serikali inafuatilia malalamiko ya hujuma ya miundombinu na vifaa katika baadhi ya maeneo na kuwashauri wawashirikishe viongozi wa vijiji katika ulinzi wa vifaa.
Social Plugin