Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ametoa muda wa siku 10 kwa wakandarasi walioshinda zabuni za kutekeleza Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili kuanza kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme.
Waziri Kalemani alitoa agizo hilo tarehe 17/05/2021 wakati akizndua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Kijiji cha Mpakali kilichopo Wilaya ya Mbogwe katika Mkoa wa Geita.
Dkt. Kalemani alisema Serikali imetenga Shilingi bilioni 75.6 kwa ajili ya kupeleka umeme katika vijiji 97 ambavyo havina umeme katika Mkoa wa Geita.
“Vijiji vyenye umeme ni 377 kati ya vijiji 474 n katika Wilaya ya Mbogwe vijiji visivyo na umeme ni 33 na tumewaletea mkandarasi atakayekamilisha kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa Serikali imetoa muda wa miezi 18 kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kusambaza miundombinu ya umeme vijijini na kuwa muda huo hautaongezwa.
Aliwataka REA kuwasimamia wakandarasi wakamilishe miradi kwa wakati kwa mujibu wa mikataba.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Martha Mkupasi alisema kuwa Umeme ni nishati muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuwa itasaidia katika kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kama vile afya na elimu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Mhe. Nicodemus Maganga alisema kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme katika jimbo hilo utafungua fursa ya uwekezaji wa viwanda vya kusindika mpunga, dengu na karanga ambazo zinalimwa ukanda huo.
Social Plugin