Na Munir Shemweta
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amejitwisha mzigo wa wananchi waliowasilisha kwake malalamiko ya fidia kwenye maeneo mbalimnbali nchini kupitia Program ya Funguka kwa Waziri kwa kuamua kuchukua hatua ya kuandika barua za madai kwa taasisi na idara zinazodaiwa fidia.
Hatua hiyo inafuatia wananchi wanaodai fidia kuzingushwa kupatiwa fidia ya maeneo yao yaliyotwaliwa kwa shughuli mbalimbali za maendeleo na kuamua kuwasilisha malamiko kwa Waziri wa Ardhi kupitia fomu maalum za Funguka kwa Waziri.
Akizungumza katika kipindi Maalum cha Funguka kwa Waziri kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC ONE tarehe 15 Mei 2021 saa tatu usiku, Lukuvi alisema, uchambuzi wa malalmiko/ migogoro ya matumizi ya ardhi iliyowasilishwa kwake kupitia Fomu za Funguka ulionesha malamiko mengi yapo kwenye masuala ya fidia.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, katika uchambuzi huo asilimia 39.4 ya malalamiko inaonesha yako katika masuala ya fidia huku uvamizi wa maeneo ukiwa na asilimia 29.4, migogoro ya kifamilia asilimia 22.9 na ile iliyopo mahakamni asilimia 5.5 na malalamiko ya milki na upimaji pandikizi ikiwa ni asilimia 2.8.
‘’Rais alishatoa maelekezo wote waliochukua ardhi ya wananchi lazima walipe fidi, wote waliorudisha fomu za Funguka kwa Waziri kwangu mimi nimechukua uwakili na nitaandika barua kwa kila anayedaiwa fidia iwe Mkurugenzi, Katibu Mkuu au Mkurugenzi wa TANROADS’’ alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi ambaye alikuwa akimjibu mwananchi kutoka mkoani Arusha Hassan Othman Shao aliyelalamikia serikali ya kijiji cha Ngabodo kuchukua eneo lake bila kufuata utaratibu wa kulipa fidia alisema, suala la fidia kwa wananchi wanaochukuliwa maeneo yao siyo la hiari bali ni matakwa ya kisheria na limetamkwa pia katika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na linatakiwa kutekelezwa kwa wakati.
‘’ Napenda niwaambie wote wanaofikiri kulipa fidia ni hiari, hakuna mali itakayochukuliwa bila fidia na ipo sheria ya utwaaji ardhi na ardhi inapotwaliwa, mtwaaji anatakiwa kulipa fidia kwa mmiliki wa asili na fidia lazima iwe kamilifu na kulipwa kwa wakati, iwe kwenye migodi, barabara au uendelezaji wowote lazima walipe fidia’’ aliongeza Waziri Lukuvi
Akielezea Programu Maalum ya Funguka kwa Waziri, alifafanua kuwa ofisi yake tayari imeanza program hiyo awamu ya pili baada ya ile ya kwanza kuonesha mafanikio makubwa na kueleza kuwa katika awamu ya pili ya zoezi hilo, fomu zilisambazwa kwa wananchi kupitia ofisi za Kata, Vijiji na Mitaa na kufanyika chini ya uratibu wa Ofisi za Ardhi za Mikoa na Halmashauri zake.
Alisema, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2021 jumla ya fomu zilizochukuliwa na wananchi zilikuwa 24,442 ambapo fomu zilizojazwa ni 3,171 na hadi sasa malalamiko yaliyokwisha fanyiwa kazi ni 1,144 ikiwemo wananchi husika kupatiwa barua za namna lalamiko/mgogoro ulivyomalizika na hiyo ni katika mikoam mbalimbali.
Katika majibu yake kwa wananchi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ikiwemo Fidia, Ufutaji Miliki za ardhi, Uvamizi wa Maeneo,Mdalali wa ufuatiliaji malalamiko, Utapeli katika masuala ya ardhi, Mauziano ya Ardhi yanayofanyika kienyeji, Makubaliano binafsi yanayozusha migogoroo ya ardhi, Mipango Miji pamoja na Urasimishaji.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin