WAZIRI MKUU AKABIDHI MAGARI 184 KWA HALMASHAURI NCHINI
Saturday, May 22, 2021
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekabidhi jumla ya magari 184 kwa maafisa elimu wa Halmashauri ikiwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya sita ya kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini.
Hafla hiyo imefanyika jana (Mei 21, 2021) katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kibasila, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Mkuu amezitaka Halmashauri zilizopokea magari zizingatie taratibu za serikali katika matumizi na matengenezo ya magari hayo.
“Magari haya mmekabidhiwa, maafisa elimu na wakurugenzi wa Halmashauri, tukute gari limepaki kisa limekosa ‘Service’ utakuwa umekosa kazi, lazima tuambizane ukweli, magari haya lazima yafanye kazi kwa zaidi ya miaka mitano hadi sita”
Amesema kuwa magari hayo ni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ufuatiliaji na tathmini kwa Maafisa Elimu, na yametolewa na Serikali ili yasaidie kuharakisha shughuli za utekelezaji wa majukumu katika sekta ya elimu.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu tawala wa mikoa kuchukua hatua ikiwa magari hayo yatatumika tofauti na malengo yaliyotarajiwa “hakikisheni magari haya yanakwenda kutekeleza shughuli za elimu kwenye halmashauri zenu na si vinginevyo”
Kadhalika Waziri Mkuu amewaagiza Maafisa elimu na wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kila kwenye shule ya Sekondari wanakamilisha ujenzi wa maabara ili kila shule iweze kupatiwa vifaa vya maabara.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka viongozi waliopo katika Halmashauri nchini kushughulikia kwa nguvu zote tatizo la utoro lengo ni kuhakikisha kila mtoto anayeanza shule anamaliza.
“Mtoto wa kitanzania kwenda shule sio hiari ni lazima, na tutawachukulia hatua kali wote wanaozuia watoto wao kwenda shule”
Waziri Mkuu pia amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na Washirika wa Maendeleo pamoja na wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Ummy Mwalimu amesema Magari hayo yamenunuliwa na Serikali kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Sekta ya Elimu (EP4R) kwa gharama ya shilingi bilioni 16.4.
Amesema kuwa hii ni awamu ya pili ya ununuzi wa magari baada ya awamu ya kwanza ambayo magari 26 yalinunuliwa kwa ajili ya usimamizi wa elimu katika ngazi ya Mikoa.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin