Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Prof.Kitila Mkumbo,akizungumza bungeni leo Mei 22,2021 wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2021/2022.
Na.Alex Sonna, Dodoma.
Wizara ya Viwanda na Biashara imewasilisha bungeni makadirio ya matumizi kwa Wizara hiyo kwa mwaka 2021-2022 na kueleza kuwa katika makadirio hayo yamelenga katika kupanua wigo wa upatikanaji wa viwanda hasa vya sukuari ili kupunguza uhaba wa sukari ambapo hutokea mara kwa mara.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha bajeti hiyo Bungeni leo Mei 22, 2021 Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema wamejipanga kukabiliana na upungufu wa sukari kwa kuanzisha viwanda vipya na kupanua uwezo wa viwanda vilivyopo kwa sasa.
“Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kupanua na kuongeza uwezo wa viwanda vikubwa vilivyopo, ikiwemo Kiwanda cha Sukari cha Kilombero,pamoja na kuanzisha viwanda vikubwa vipya,
“Sambamba na hatua hizi, katika jitihada za kuongeza uzalishaji wa sukari ili kukidhi mahitaji ya bidhaa hii nchini, Serikali imeelekeza Taasisi ya TEMDO kufanya usanifu na kuanza kutengeneza mitambo midogo kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali wadogo waanze kuchakata miwa ili kupata sukari (Sugar Min –Processing Plant)” amesema Mkumbo.
Amesema kuwa hatua hii itaweza kuongeza uzalishaji wa sukari na kuhakikisha kuwa wakulima wadogo (out growers) wanaweze kuchakata miwa yao bila kuwa tegemezi katika viwanda vikubwa.
Pia amesema watakamilisha taratibu za kuwapata wawekezaji wapya waviwanda vilivyobinafisishwa na baadaye kurudishwa serikalini, kukamilisha kanzidata ya viwanda na biashara nchini, kuimarisha mfumo wa usajili wa makampuni na leseni za biashara kupitia Wakala wa Usajili na Leseni za Biashara (BRELA).
Vipaumbele vingine ni kuimarisha Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza wajasiriamali Wadogo(National Entrepreneurship Development Fund-NEDF) kwa kupanua wigo wa mtaji wa mfuko huo, kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa maeneo maalum ya kibiashara (trading hubs).
Ameongeza kuwa “Vipaumbe vingine ni kuimarisha na kukuza matumizi ya utafiti na maendeleo, teknolojia na ubunifukatika sekta ya viwanda na biashara, kuendelea kusimamia viwango vya ubora na kubuni viwango vipya kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa Tanzania kupitia TBS na Wakala wa Vipimo (WMA)” amesema.
Vipaumbele vingine ni kuhamasisha, kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha chuma na bidhaa za chuma, kuendeleza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya ngozi, nguo na mavazi, kuhamasisha, kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha chuma na bidhaa za chuma.
Kuweka msukumo na mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya kuunganisha vifaa vya kielekroniki na magari, kuhamasisha viwanda vinavyozalisha vifaa vya ujenzi.
Pia amebainisha kuwa Serikali imejipanga katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza betri na umeme wa magari kwa kutumia rasilimali asili za nchi kama vile madini ya Lithium, Vanadium na Titanium, ambayo pia yanapatikana hapa nchi.
Vile vile tutajikita kuweka mazingira wezeshi kisera na kisheria ya kufanya biashara, kujiunga au kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika jumuiya za kiuchumi na kimasoko za kikanda kwa ajili ya kupanua fursa za kibiashara kwa bidhaa za Tanzania ambazo zitazalishwa hapa nchini.
Waziri Mkumbo ameongeza kuwa “Pia tutajikita katika kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali na wafanya biashara wadogo ili wapanue mitaji yao ili kuendesha biashara zao, tutaweka mazingira bora kisera, kisheria na kiutendaji kwa ajili ya kuchochea na kulinda ukuaji wa sekta binafsi kama injini na msingi wa ujenzi wa uchumi wa viwanda na shindani kuweza kushindana na mataifa mengine” amesema.
Ameongeza kuwa “Lengo kuu la ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ni kuleta mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu, moja ya nyenzo ya kuleta mapinduzi ya uchumi iliyoanishwa katika ilani hiyo ni kujenga Tanzania ya uchumi wa viwanda na kukuza biashara” amesema.
Wizara ya Viwanda na Biashara imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi Shilingi bilioni, 105,670,459,000, kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni, 52,582,573,000, ni za Matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 53,087,886,000, ni za Matumizi ya Maendeleo.
Social Plugin