MAPENDEKEZO MUHIMU BAJETI KUU YA SERIKALI 2021/2022

 Serikali imebainisha maeneo muhimu  ya kipaumbele kwa mwaka 2021/22 ikiwamo kupunguza kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane.

Pia kuanzia sasa madiwani watalipwa posho moja kwa moja na Serikali kuu huku ikitenda Sh bilioni 328.2 kwa ajili ya kugharamia Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Hayo yameelezwa jana  Bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati wa kuwasilisha hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022.

1.Sensa

Amesema Tanzania inajiandaa kufanya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu SURA 351 ambapo Sh bilioni 328.2 zinatarajia kugharimu Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022.

2.Maslahi ya Wafanyakazi

Nchemba alisema katika kutambua na kuthamini mchango wa watumishi katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi,  Serikali imechukua hatua ya kupunguza kiwango cha cha chini cha kutoa kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8

 Amesema," Hatua hii ni mwendelezo wa juhudi za Serikali za kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, ambapo kiwango hicho kimepunguzwa kutoka asilimia 11 mwaka 2015/16 hadi asilimia 8 itakayoanza kutekezwa mwaka 2021/22."

3.Tozo mkopo Elimu ya Juu

Alisema pia kufuta tozo ya asilimia 6 iliyokuwa ikitozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya mkopo wa elimu ya juu kwa wanufaika na kutenga jumla ya Sh  bilioni 449 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 92,619.

4.Maslahi ya Madiwani, Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata

Dk Nchemba alisema  katika baadhi ya halmashauri madiwani wamekuwa wakikopwa posho zao na wengine kufikia hatua ya kuwapigia magoti wakaurugenzi watendaji ili walipwe.

" Hatua hii imekuwa ikipunguza ufanisi katika halmashauri zetu kwa madiwani wengi kufanya maamuzi yanayopendekezwa na wakurugenzi watendaji hata kama hayana maslahi kwa Taifa ili waweze kulipwa posho zao.

" Napenda niwaeleze kuwa Mama yetu (Rais Samia Suluhu) amesikia kilio chenu na alinielekeza mimi pamoja na Waziri wa TAMISEMI kulitafutia ufumbuzi suala hili.  Kuanzia mwaka 2021/22, Serikali Kuu ianze kulipa posho za kila mwezi moja kwa moja tena kwenye akaunti zao kwa Halmashauri zote zenye uwezo mdogo kimapato.

Alisema kwa Halmashauri 16 zenye uwezo mkubwa wa kimapato (Daraja A) zitaendelea kutumia mapato yake ya ndani kulipa posho za Madiwani kupitia kwenye akaunti zao.

Kuhusu Maafisa Tarafa, Dk Nchemba alisema pamoja na serikali kuwanunulia pikipiki, lakini wengi wameshindwa kugharamia ununuzi wa mafuta na matengenezo  hali iliyopunguza ufanisi.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuanzia mwaka 2021/22, Serikali Kuu ianze kulipa posho ya Sh 100,000  kwa mwezi kwa kila Afisa Tarafa ili waweze kumudu gharama za mafuta na matengenezo ya pikipiki.

Kuhusu watendaji kata, Dk Nchemba alisema watendaji hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu na kuwa pia wataanza kulipwa posho ya Sh  100,000 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri yaliyokuwa yakitumika kulipa madiwani.

5.Madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

Dk Nchemba amesema kumekuwepo na changamoto za muda mrefu za ulipaji wa mafao kwa wastaafu kutokana na ufanisi mdogo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika kuhudumia wastaafu wetu.

" Hali hiyo kwenye mifuko yetu 23 imechangiwa, pamoja na mambo mengine, na uwepo wa madeni ambayo mifuko inaidai Serikali na hivyo kusababisha wastaafu wetu kukosa au kusubiri kwa muda mrefu ili kulipwa mafao yao.

Alisema Serikali imejipanga kulipa madeni yanayodaiwa na mifuko kwa kutenga fedha kwenye bajeti na kutumia utaratibu wa kutoa hatifungani maalum isiyo taslimu  zitakazoiva kwa nyakati tofauti kuanzia miaka miwili hadi 25.

" Hatua hii inakwenda kumaliza kabisa tatizo hilo la wazee wetu kudai haki yao kwa damu na machozi yaliyodumu kwa muda mrefu."

Aidha, Dk Nchemba alisema serikali imepoka malalamiko ya kucheleweshwa kwa michango ya watumishi kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na baadhi ya ofisi za Serikali kutopeleka kabisa michango hiyo.

Alisema kutokana na hali hiyo, amependekeza kuanzia sasa kuanza kulipa michango hiyo moja kwa moja kutokea Hazina kwa taasisi zote ambazo watumishi wanalipwa na Hazina.

" Taasisi ambazo zinalipa watumishi kutokana na vyanzo vyao vya mapato zitaendelea kupeleka michango ya watumishi wao kwa ufuatiliaji wa karibu wa Serikali. Pia itafanya uhakiki na kulipa madeni ya michango ambayo haijawasilishwa kwenye mifuko hadi sasa.

6.Jeshi la Polisi

Dk Nchemba alisema kuanzia mwaka 2021/22 askari wa Jeshi la Polisi wataingia mkataba wa kipindi cha miaka 6 na kuingia katika ajira ya kudumu.

Alisema hatua hiyo hali ya kuchelewa kwa miaka 12 wanapopata mkatabwa wa kudumu ikilinganishwa na mtumishi aliyeingia pamoja kazini katika idara nyingine.

7.Kurahisisha Kasi ya Utekelezaji wa Miradi

Dk Nchemba alisema katika kuimarisha usimamizi na ufanisi katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango itafanya mabadiliko katika Kanuni ya 21 ya Sheria ya Bajeti, ili kuondoa changamoto iliyopo ya fedha ambazo hazijatumika hadi Juni 30 kila mwaka kurejeshwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.

Alisema fedha hizo zitawekwa kwenye Akaunti ya Amana kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli ambazo hazijakamilika wakati wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha husika.

" Kwa msingi huo, kuanzia sasa hakutakuwa na fedha zenye miadi zitakazorejeshwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ifikapo Juni 30 kila mwaka wa fedha isipokuwa pale ambapo Maafisa Masuuli wamekiuka masharti ya Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348."

8.Kodi ya Majengo

Dk Nchemba amesema kumekuwa na changamoto kubwa katika ukusanyaji wa kodi ya majengo, hali iliyosababisha Serikali kubadili njia za ukusanyaji mara kwa mara.

Amesema," Katika kuhakikisha kodi hii inafikia malengo, Serikali imeandaa utaratibu mzuri wa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi ya majengo."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post