WASHINDI WA CRDB BANK MARATHON KUZAWADIWA JUMLA YA SHILINGI MILIONI 45.4

 

Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB akionyesha bango linaloonyesha zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa washindi wa CRDB Bank Marathon 2021. Wengine pichani ni  Mkurugenzi wa Uendeshaji wa EFM, Denis Busulwa (kulia), Meneja Masoko wa Strategis, Lilian Malakasuka (wapili kulia) na Mkuu wa Kitengo cha BancAssurance Alliance General, Osward Tellis. 
 
=======  ======  ========
 
Dar es Salaam 29 Juni, 2021 – Benki ya CRDB imetangaza zawadi za washindi wa msimu wa pili wa CRDB Bank Marathon 2021 ambapo jumla ya shilingi milioni 45.4 zitatolewa kwa washindi 32. Akitangaza zawadi hizo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa alisema kwa mwaka huu zawadi zimeongezwa ili kuendana na hadhi ya kimataifa ambayo CRDB Bank Marathon ilipewa mwaka huu baada ya kusajiliwa na Chama cha Usajili na Upimaji wa Mbio za Kimataifa (AMIS) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (World Athletics).
 
“Mwaka huu sio marathon tu ni ya kimataifa, hata zawadi pia ni za kimataifa zaidi. Tumejipanga kutoa zawadi nono kwa washindi, kwa mbio kubwa za kilometa 42 mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 5, mshindi wa pili shilingi milioni 3, mshindi wa tatu shilingi mili 2 na mshindi wa nne shilingi milioni 1. Hizi ni zawadi kubwa zaidi kupata kutokea katika mbio zote nchini,” alisema Tully huku akibainisha kuwa wingi wa zawadi unatokana na kuongezeka kwa namba ya washiriki ambapo ambapo matarajio ni kupata washiriki 5,000 kutoka ndani nan je ya nchi.
Tully aliwataka Watanzania kujitokeze kwa wingi kujisajili katika mbio hizo za CRDB Bank Marathon kwani pamoja na kuwa mbio hizo sasa hivi ni za kimataifa lengo kubwa ni kukuza uzalendo miongoni mwa Watanzania kwa kuwaleta pamoja kutatua changamoto katika jamii. “Wakimbiaji wengi wa kimataifa wanajisajili ma mia kwa mamia kuja kushiriki kusambaza tabasamu nchini kwetu, lakini tungependa zaidi kuona Watanzania wakishiriki kwa wingi kwani hii ni marathon yetu na tungependa pia kuona zawadi hizi zikibaki nyumbani,” aliongezea.
 
Akizungumzia fursa zitokanazo na mbio hizo ambazo sasa hivi zimesajiliwa kimataifa, Tully alisema mbio hizo zitakwenda kuchochea uchumi wa Jiji la Dar es Salaam na kulitangaza jiji hilo pamoja na Tanzania kwa ujumla duniani kote. Alisema mbio hizo zitatumika kutangaza vivutio na historia ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo utamaduni wa pwani (swahili culture). “ Pamoja na hivyo mbio hizi pia zitasaidia kuonyesha vipaji vya wakimbiaji duniani kwani mbio hizi zitaonyeshwa live na TVE ambayo ipo DSTV. Tunakwenda kufunguka zaidi kwenye anga za dunia,” alisisitiza Tully.
Akikumbushia lengo la kuandaa marathon hiyo, Tully alisema mbio hizo zinalenga kuwaleta pamoja Watanzania kuchangia watu wenye uhitaji katika jamii pamoja na kutatua changamoto nyengine zinazoikabili jamii. Alisema mwaka huu lengo ni kukusanya shilingi milioni 500 ambazo zitaelekezwa katika kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ujenzi wa kituo cha mawasiliano “Call Center” katika Taasisi ya Kansa ya Ocean Road na kampeni ya utunzaji mazingira ya “Pendezesha Tanzania” ambapo miti milioni 1 inatarajiwa kupandwa ndani ya miaka 3.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa EFM na TVE, Denis Busulwa (Ssebo) alisema kampuni yao inajivunia kuwa washirika wa CRDB Bank Marathon kutokana na mbio hizo kujikita zaidi katika kuhamasisha watu kusaidia jamii. “Tunaishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizi zinazowaleta Watanzania kushiriki katika kutatua changamoto katika jamii. EFM na TVE ni vyombo vya habari vya jamii hivyo tunakila sababu ya sisi kushiriki katika mbio hizi ikiwa ni sehemu yetu ya kusaidia jamii,” alisema Ssebo huku akihamasisha Watanzania kujisajili kwa wingi.
 
Naye Katibu Mkuu wa Shirikikisho Riadha Tanzania, Jackson Ndaweka aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizo kwa viwango vya kimataifa huku akimhakikishia Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa kuwa zawadi zote zitabaki nchini kwani wanariadha sasa hivi wanajifua kuelekea tarehe 15 Agosti 2021 siku ya marathon. “Wanariadha wetu wana kiu kubwa ya kushindana baada ya mbio nyingi za kimataifa kuahirishwa kutokana na changamoto ya COVID-19. Zawadi hizi zimekuja wakati muafaka na wanariadha wetu wapo wanajifua kuchuana na wanariadha wa kimataifa,” alisema Ndaweka.
Hafla hiyo ya kutangaza zawadi ilihudhuriwa washirika mbalimbali wa CRDB Bank Marathon ikiwamo kampuni za bima za Sanlam, Alliance (Life na General), Heritage, Mayfair na Britam, pamoja na viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) na klabu za riadha Dar es Salaam. Viongozi hao walipongeza juhudi zinazofanywa na Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Marathon na kuahidi kuendelea kushirikiki katika mbio hizo.
 
Kujisali na kuchangia katika CRDB Bank Marathon washiriki wanatakiwa kutembelea katika tovuti rasmi yam bio hizo www.crdbbankmarathon.co.tz ambapo mtu binafsi anatakiwa kuchangia shilingi 30,000 na washiriki kupitia vikundi ni shilingi 25,000. Malipo yanaweza kufanyika kupitia matawi ya Benki ya CRDB, CRDB Wakala, SimBanking App, mitandao ya simu na kupitia kadi ambazo zinawawezesha hadi watu wa nje ya nchi kufanya malipo. 


 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post