Muyengi alisema katika Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa miaka 10 2020/2021 hadi 2029/2030 ambao ulizinduliwa mwezi Septemba mwaka jana Serikali imeka lengo la kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi wote zikiwemo huduma za bima.
“Nafahamu Benki ya CRDB mnauzoefu mkubwa katika huduma za bima kulinganisha na wengine, kwani nyie mlianza na kampuni ya udalali ambayo imekuwa ikifanya vizuri. Tumieni uzoefu huo kuboresha zaidi kwa maana ya kuja na bidhaa na njia bunifu za ufikishaji huduma za bima kwa kushirikiana na makampuni ya bim,” aliongezea Muyengi huku akipongeza ubunifu wa huduma za bima za KAVA Assurance na Bima ya Vyombo vya Moto kidijitali kupitia SimBanking zinazotolewa na Benki ya CRDB na makampuni washirika ya bima.
Akizungumzia kuhusu suala la elimu ya bima kwa umma, Muyengi alisema Serikali kupitia Sheria ya Bima imeelekeza kuwa taasisi zote zinazotoa huduma za bima zinapaswa kuhakikisha wafanyakazi wake wanaohusika kutoa huduma hizo wanapata mafunzo ya mara kwa mara, kuwasilisha mpango wa elimu ya bima kwa umma na kutenga bajeti ya utekelezaji.
“Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kutimiza takwa hili la kisheria, mpango wenu wa elimu ya bima kwa umma tumeupokea na kuupitisha na leo hii mmetuita kuja kuona jinsi mnavyokwenda kutekeleza kwa vitendo, hongereni sana,” alipongeza Muyengi huku akiitaka Benki ya CRDB kutoishia kutoa elimu hiyo katika matawi na kwenda mpaka kwa wananchi kupitia makongamano ya elimu.
“Tukiwa Benki ya kizalendo tunaamini tunawajibika katika kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunafikia ujumuisha wa bima kwa asilimia 50 kama ambavyo imeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha,” alisema Nsekela ambapo alisisitiza kuwa kuskosekana kwa elimu ni moja ya sababu kubwa ya kuwa na matumizi madogo ya bima nchini.
Nsekela alisema kupitia kampeni hiyo Benki ya CRDB imejipanga kutoa elimu ya bima kupitia warsha za elimu ambao zitaendeshwa na Benki hiyo nchi nzima, vilevile Benki hiyo imejipanga kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha elimu hiyo inafika kila kona ya nchi.
“Hivi karibuni pia tutakwenda kutazindua kampeni yetu ya Tupo Mtaani Kwako kwa mwaka 2021, kampeni hii pia itahusisha elimu ya bima. Hivyo niwaombe Watanzania wanapowaona wafanyakazi wetu mtaani wasisite kuuliza maswali kwani sisi tumejipanga kikamilifu kuwapa elimu ya bidhaa zetu ikiwamo bima,” aliongezea Nsekela.