BENKI YA CRDB YAZINDUA AKAUNTI YA 'HODARI' KWA AJILI YA WAJASIRIAMALI KWENYE UZINDUZI WA MSIMU WA PILI WA KAMPENI YA TUPO MTAANI KWAKO

 


Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Wateja wa Kati na Wadogo wa Benki hiyo, Boma Raballa, Meneja wa Benki hiyo Kanda ya Mashariki, Badru Idd na Maafisa Waandamizi wa Benki ya CRDB wakipeperusha bendera kuashiria uzinduzi wa kampeni ya TUPO MTAANI KWAKO awamu ya pili iliyo boreshwa zaidi ikienda sambamba na Uzinduzi wa Huduma mpya ya HODARI AKAUNTI ambayo ni mahususi kwaajili ya wajisiriamali na wafanya biashara wadogo nchini, ambao wataunganishwa moja kwa moja na huduma ya LIPA HAPA. Uzinduzi huu umefanyika leo kwenye viwanja vya Mbagala Zakiem, Dar es salaam ikiwa ni jitihada za makusudi kabisa za Benki ya CRDB kuhakikisha inalifikia kila kundi kwa kadiri ya mahitaji yake na kuwapa usalama na urahisi katika ufanyaji wa biashara zao.

Benki ya CRDB leo imezindua akaunti ya wajasiriamali iliyopewa jina la “Hodari,” ikiwa na lengo la kuwasaidia wajasiriamali katika sekta mbalimbali nchini kuboresha biashara zao. Uzinduzi wa akaunti hiyo umeenda sambamba na uzinduzi wa msimu wa pili wa kampeni ya Tupo Mtaani Kwako” inayolenga kuhamasisha matumizi ya huduma za benki pamoja na kuwapa Watanzania elimu ya fedha na uwekezaji.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao ulifanyika katika viwanja vya Mbagala Zakhiem jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile alisema akaunti hiyo ya “Hodari” itakwenda kusaidia kurahisisha biashara za wajasiriamali kwa kuwawezesha kuweka akiba kwa urahisi, kupokea malipo kidijitali kupitia CRDB Lipa Namba na kuunganisha na fursa za uwezeshaji kupitia mikopo ya wajasiriamali.

Bruce alisema pamoja na kuboresha biashara za wajasiriamali, akaunti hiyo pia inakwenda kuleta unafuu mkubwa kwao kwani wateja hawata tozwa makato yoyote kwa miamala ambayo itafanyika ndani ya mtandao wa Benki ya CRDB kuanzia kwenye matawi, CRDB Wakala, ATMs na SimBanking. Alisema akaunti hiyo pia itakuwa ikifunguliwa bure ili kuweza kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi hususani wale wenye mitaji midogo.

Uzinduzi wa akaunti ya “Hodari” unakuja wiki chache baada ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhimiza taaasisi za fedha kuja na mikakati ya uwezeshaji kwa wajasiriamali ambao wengi wao ni vijana. Bruce anasema uzinduzi wa huduma hiyo ya “Hodari” ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais, huku akibainisha kuwa malengo ya Benki hiyo nikuwafikia wajasiriamali kote nchini.

Nichukue fursa hii kuwaalika wajasiriamali wote kufungua Akaunti ya Hodari na kuanza kufurahi faida hizi nilizozitaja hapa. Huduma hii ni kwa wajasiriamali wote iwe bodaboda, mama/ baba lishe, wauza genge, wenye maduka ya reja reja, wamachinga na wengineo, wote hawa kwetu ni Hodari na ujumbe wetu leo ni tunawaalika kuwa mahodari, alisema Bruce.

Uzinduzi wa akaunti hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa maoni ambayo benki hiyo ilipokea kutoka kwa wateja wake katika msimu wa kwanza wa kampeni ya “Tupo Mtaani Kwako,” mwaka jana. Akitaja maboresho mengine ambayo yamefanyika kutokana na maoni ya wateja katika kampeni hiyo, Bruce alisema mapema mwaka huu benki hiyo ilizindua huduma ya SimBanking iliyoboreshwa zaidi ambayo inawawezesha wateja kujifungulia akaunti wenyewe, na kupata huduma za bima na mikopo kidijitali.

Katika kampeni ya mwaka jana vilevile tulipata mrejesho kuhusu bima, ambapo hivi karibuni Benki yetu ilizindua kampeni maalumu ya elimu ya bima kwa umma yenye kauli mbiu ya “Furahia Maisha.. Bima Unachokithamini, jitihada zote ni matokeo ya kufanyia kazi maoni ya wateja wetu na wananchi kwa ujumla, alisisitiza Bruce huku akibainisha kuwa kampeni ya mwaka ilifanikiwa kufika katika mikoa 20 na kufikia zaidi ya watu laki 1.

Akizungumzia dhumuni la kuifanya kampeni hiyo ya “Tupo Mtaani Kwako kwa msimu wa pili, Bruce alisema wananchi wengi walipendekeza elimu ya huduma za benki kuendelea kutolewa kutokana na watu wengi kuwa na uelewa mdogo unaopelekea kuwa nje ya mfumo rasmi wa kibenki. “Tukiwa Benki ya kizalendo tunajukumu la kuhakikisha wananchi wote wananufaika na huduma za kibenki, hivyo tukaona ni vyema tukaifanya kampeni hii kuwa endelevu ili kusaidia lengo la Serikali la kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini ,” alisema Bruce.

 

Katika kampeni ya “Tupo Mtaani Kwako” ya mwaka huu Benki ya CRDB imejipanga kutumia timu ya wafanyakazi wake wabobevu katika masuala ya kibenki kuwatembelea wateja popote pale walipo, iwe ni ofisini, sokoni, dukani, stendi na kuwapatia huduma.

“Tutakuwa tukitumia magari yetu haya ambayo mnayaona hapa kuwafikia wateja mtaani, lakini pia tutakuwa na MaGazebo ambayo yatakuwepo mtaani kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wateja,” aliongezea Bruce huku akiwataka wateja kutumia fursa hiyo ya kusogezwa kawa huduma karibu kufungua akaunti na kuweka akiba.

Bruce amesema amesema kampeni hiyo pia inalenga katika kuhamasisha matumizi ya njia mbadala za utoaji huduma ikiwamo CRDB Wakala, SimBanking, Internet Banking na TemboCard. Kupitia njia hizi mteja anaweza kufanya miamala yake ya benki popote pale alipo kwa urahisi, usalama na unafuu.

“… hadi kufikia sasa tuna CRDB Wakala zaidi 20,000 nchi nzima ambao wanatoa huduma mtaani, kwahiyo tunaposema Tupo Mtaani Wako, pia tunamaanisha huduma za kibenki karibu zaidi na mteja kupitia CRDB Wakala,” alisisitiza Bruce huku akibainisha kuwa katika kampeni hiyo wateja watakuwa wakiunganishwa na huduma za SimBanking, Intenert banking na TemboCrad Visa, MasterCard na UnionPay.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post