Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Desdelius Haule kushoto na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Juma Mnwele kulia wakichimbua kisiki katikati eneo la mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri inayojengwa katika kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera ambapo Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 500. Picha na Muhidin Amri
**
Na Muhidin Amri - Mbinga
Serikali imeipatia Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya ya Mbinga ikiwa ni mkakati wa kuimarisha na kuboresha huduma za afya katika Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wilaya ya Mbinga Juma Mnwele amesema, tayari wamepokea fedha hizo kutoka Serikali Kuu na wameshaanza kujenga Hospitali hiyo katika kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera.
Mnwele amesema, ujenzi wa Hospitali hiyo utafanyika kwa awamu kulingana na fedha zitakazoletwa na Serikali na kwa kuanzia wataanza kujenga majengo ya vipaumbele kama jengo la wagonjwa wa nje(OPD) na maabara na kichomea taka na majengo mengine yataendelea kujengwa kulingana mapato.
Amesema, kwa kazi zilizofanywa na wananchi wa Kigonsera kusafisha eneo zimesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zitasaidia kuongeza majengo mengine ya kutolea huduma na kuwaomba wananchi hao kuendelea kufanya kazi za kujitolea katika mradi huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinda Desdelius Haule, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutao fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hiyo na miradi mingine ya maendeleo inayokwenda kuharakisha kukua kwa uchumi.
Amesema, ujenzi wa Hospitali hiyo ni matokeo mazuri ya utendaji wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi ikiwa ni sehemu ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho kuimarisha na kuboresha huduma za Afya kwa wananchi.
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali Kuu,Serikali ya kijiji cha Kigonsera,imetoa zaidi ya ekari 35 za ardhi ili kujenga Hospitali hiyo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Emanuel Ngongi amesema, kwa kutambua changamoto walizokabiliana nazo kwa muda mrefu serikali ya kijiji kupitia mkutano Mkuu wa kijiji uliowajumuisha wananchi wote umeridhia kutoa ardhi iliyotengwa baada ya Halmashauri ya wilaya kuwa na wazo la kujenga Hospitali.
Ngongi amesema, wameamua kutoa ardhi hiyo bure ili kutekeleza mradi huo ambao unakwenda kumaliza changamoto ya huduma za afya kwa wakazi wa kijiji hicho ambao sasa wanalazimika kwenda hadi Hospitali ya Misheni Peramiho na Hospitali ya Rufaa Songea mjini umbali wa km 100 kufuata huduma ya matibabu.
Amesema, ni heshima kubwa na fursa pekee kuona Halmashauri ya wilaya imeamua kujenga Hospitali kubwa katika kijiji hicho na kuishukuru serikali ya awamu ya sita kutoa fedha za ujenzi wa Hospitali hiyo.
Mtendaji wa kijiji hicho Kasiana Kapinga amesema, uwepo wa Hospitali ya wilaya katika kijiji hicho utasaidia sana wananchi hasa wale wenye kipato kidogo kupata matibabu karibu na hivyo kuokoa maisha yao hususani mama wajawazito pindi wanapotaka kujifungua.
Amesema wananchi wa kijiji hicho wamepokea mradi huo kwa furaha na wameshiriki katika kazi za kusafisha eneo la ujenzi kwa kukata miti na kung’oa visiki wakiwa na matumaini kwamba kujengwa kwa Hospitali hiyo ni sehemu ya chachu ya kuharakisha maendeleo yao.
Alisema, kwa sasa wakazi wa kijiji hicho wanalazimika kupata huduma za matibabu katikazahanati ya kanisa katoriki Kigonsera kwa gharama kubwa na wengine kwenda nje ya wilaya ya Mbinga jambo linalorudisha nyuma maendeleo kwa kupoteza muda mwingi ambao wangeutumia kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa kazi nzuri wanazofanya katika kutekeleza kazi za maendeleo na miradi mbalimbali inayokwenda kuchochea na kuhamasisha wananchi kufanya kazi za kujitolea.
Ameitaka Halmashauri hiyo kuangalia uwezekano wa kuongeza majengo mengine, badala ya kujenga majengo matatu hasa kutokana na ushiriki mkubwa wa wananchi katika ujenzi huo.
Amesema, kama watajipanga vizuri fedha hizo zinaweza kujenga majengo mengi ya kutolea huduma za afya na kuhakikisha majengo yatakayojengwa yanakuwa na ubora mkubwa na yanakamilika haraka.
Nshenye,amewataka wananchi wa kijiji hicho kutumia uwepo wa Hospitali hiyo kujenga nyumba bora kwa ajili ya watumishi na kuboresha huduma mbalimbali kwa ajili ya jamii itakayoishi kuzunguka eneo hilo, badala ya kuwa waangaliaji kwa watu kutoka nje ya wilaya hiyo.
Social Plugin