Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga (kulia) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Bilinith Mahenge kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani
Mweka hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bw. Revcatus Mohabe akisoma taarifa ya hoja ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza kwenye kikao Maalum wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. kikao hicho kililenga kujadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30,2020
*****
Na Edina Alex,Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa hatua ya ukusanyaji wa mapato kwa kiwango cha juu, sambamba na kuibuka kinara kwa kupata hati safi kwa miaka saba mfululizo.
Mahenge ametoa pongezi hizo leo kwenye Kikao Maalum wa Baraza la Madiwani lililokutana kujadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 ,2020."Nilipofika na kupewa taarifa za maendeleo ya mkoa nikaona Halmashauri hii ya Ikungi mmekusanya mapato kwa asilimia 82 na mmestahilishwa hati hii safi kwa mfululizo wa miaka yote Saba, hongereni sana," alisema Mahenge.Katika hilo aliwataka kuongeza jitihada mara mbili zaidi ili kuifanya Halmashauri hiyo kuwa namba moja kitaifa, na hatimaye kuleta chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwa wana-Ikungi na Singida kwa ujumla.Kwa upande wake Mkaguzi wa ndani Mkoa wa Singida, Naomi Kalinga amepongeza Halmashauri hiyo kwa kuweza kufanyia kazi kikamilifu hoja za ukaguzi kwa kuzipunguza kutoka 71 hadi 26 suala ambalo ni kiashiria kuwa kuna kazi kubwa imefanyika kama timu ya pamoja.Aliwataka kuendelea na moyo huo ili kuifanya Ikungi kuwa mahali salama pa kufanyia kazi, na kubwa kuhakikisha hoja zilizofungwa hazijirudii tena.Naye Mkaguzi Mkuu Mkoa (CAG) Nkanyila Makawa mbali ya kupipongeza Halmashauri ya Ikungi amewataka waendelee kufuata sheria za matumizi ya fedha za Serikali"Ikungi mnajitahidi sana kuzifuata sheria na taratibu za matumizi ya fedha za Serikali,nawasihi sana msibweteke na sifa hizi...maana mgema akisifiwa tembo hutia maji.Tambueni kuwa kila mnachokifanya nyuma yenu kuna jicho la pili," alisema Makawa.Pamoja na hayo Mahenge alisisitiza kuwa anataka kila chanzo cha mapato ndani ya Halmashauri kichangie asilimia 100 kwa usimamizi wake.Aidha alihamasisha sekta ya kilimo kujipanga vilivyo kwenye eneo la kilimo hususani kilimo cha alizeti,ili kuufanya Mkoa wa Singida kuwa suluhisho la mahitaji ya upatikinaji wa kutosha wa mafuta ya kula ambayo yanatumia fedha nyingi kuagizwa kutoka nje."Ninaomba Halmashauri zote za Mkoa huu anzeni kutenga maeneo makubwa kwa ajili ya wawekezaji kwenye zao la alizeti. Kwa sasa nguvu kubwa ya serikali kwenye zao hili imeelekezwa kwenye mikoa mitatu ikiwemo Singida." alisema Mahenge
Social Plugin