Wakati Presha ya Uteuzi wa Wakuu wa Wilaya ikiendelea kupanda, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Mkuu wa wilaya ya Morogoro Bakari Msulwa pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri ya Morogoro, Bi. Sheilla Lukuba ambako Wafanyabiashara wadogo waliondolewa kwa nguvu hivi karibuni.
Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza uamuzi huo leo Juni 15,2021 mkoani Mwanza wakati wa mkutano wake na Vijana wa Tanzania kupitia vijana wa mkoa huo.
Rais Samia amesema amesikitishwa na kitendo cha kuondolewa kwa nguvu kwa Wafanyabiashara hao, na kwamba kama ingekuwa ni lazima Wafanyabiashara hao kuondolewa ingetumika njia nyingine na si nguvu na kuharibu bidhaa zao.
Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Wafanyabiashara hao walitengewa eneo la mbali kwa ajili ya kufanya biashara zao na walipoona hakuna biashara waliamua kurudi maeneo ya mjini na ndipo walipoanza kuondolewa kwa nguvu.
Wakati hayo yakiendelea Rais Samia Suluhu Hassan amesema atafanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya hivi karibuni na atawapa nafasi zaidi vijana akibainisha kuwa kipindi hiki ni cha vijana kusimamia maendeleo ya nchi.
“Kuna mkeka wa ma Dc (wakuu wa wilaya) utakaotoka hivi karibuni..., ninataka kuwaambia wote ni vijana. Kwa hiyo hizo ndizo fursa mlizonazo vijana ingawa baadhi yenu tunavyowapa fursa hizi mnakwenda kufanya mnayofanya na mnatuangusha” amesema Rais Samia.
Aidha amewataka vijana wanaopata fursa hizo walitumikie Taifa kwa umakini na ufanisi.
“Sisi viongozi wenu kazi yetu kuonesha njia vijana wapite na muendelee na safari ya maendeleo lakini pia kulilinda na kuendeleza Taifa hili”,ameongeza.
Amesema hata baraza la mawaziri wengi ni vijana sambamba na wakuu wa mikoa na makatibu tawala wengi ni vijana.