Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Ummy Mwalimu ameagiza wakuu wa mikoa kuwaapisha Wakuu wa Wilaya wote walioteuliwa jana Jumamosi Juni 19,2021 na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuanzia kesho Jumatatu Juni 21, 2021 na endapo watachelewa sana basi wafanye Jumanne Juni 22,2021.
Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo Jumapili Juni 20, 2021 muda mchache baada ya kumaliza ziara yake yake ya kukagua ujenzi wa stendi ya mabasi ya Mwenge jijini Dar es salaam.
"Kesho Jumatatu wote waanze mchakato wa kuwaapisha Wakuu hawa wa Wilaya. Kusiwe na kisingizio chochote, kama kuna sababu basi Jumanne mchakato huu ukamilike ili Jumatano waanze kazi mara moja",amesema.
“Waende wakaripoti kwenye vituo vyao vya kazi kwanza kisha baadaye warudi kwa ajili ya utaratibu wa kuhama. Wakuu wa Mikoa wote warudi kwenye vituo vyao vya kazi kwa ajili ya kuwaapisha Wakuu Wilaya wamechelewa sana basi wafanye Jumanne”, ameongeza Waziri Ummy.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy wakuu wa wilaya walioteuliwa jana ni 139 kati yao 56 wapya na 83 wamebaki. kati ya 83 waliobaki, 26 wamebakishwa kwenye vituo vyao huku wengine wakihamishwa katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha utendaji.
Social Plugin