Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge
Na Edina Malechela,Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge ameagiza Halmashauri zote za Mkoa huo kuanisha na kuwajibika ipasavyo katika kusimamia vyanzo vyote vya mapato ili kuhakikisha kila chanzo kinachangia kwa asilimia 100.
Dkt. Mahenge aliyasema hayo leo kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Singida lililokutana kujadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2020.
"Kama tunakusanya Shilingi milioni mia 286 tunapaswa kujiuliza huo ndio uwezo wetu kwenye chanzo husika? lazima tujiwekee utaratibu wa kuwajibishana kwa wahusika wa eneo hilo watakao fanya vibaya", alisema Mahenge.
Akizungumza ajenda ya alizeti aliagiza kila Halmashauri kujipanga kwa kampeni hiyo na kuhamasisha fursa zote zilizopo kwenye zao Hilo ambalo mahitaji yake yanafikia tani laki 650,000 ili kutoshereza mahitaji nchi nzima .
"Singida tumeomba ruzuku ya mbegu ya alizeti kiasi cha tani 1500 sanjari na maafisa ugani wanaotarajiwa kusambazwa kwenye vijiji na kata mkoani hapa, hivyo niwasihi sana wana Singida changamkieni fursa hii ya kilimo cha alizeti",alisema Mahenge.
Katika hatua nyingine Mahenge waliwataka watendaji wa Halmashauri kuheshimu sheria za matumizi ya Fedha ili kupunguza hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu zisizokuwa za lazima.
Hata hivyo, Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Nyigana Mahende alipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa kufanikiwa kupunguza hoja kutoka 66 hadi kufikia 27, jambo linalothibitisha kuwa kuna kazi kubwa imefanyika.
Aliwahimiza kuendelea kuwa waaminifu na kuchapa kazi bila ya kuruhusu hoja zilizofungwa kujirudia ili kuifanya Halmashauri ya Singida kuwa mfano kiutendaji.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Elia Digha alisema juhudi mbalimbali zinaendelea kuhakikisha wanaondoa kabisa hoja zilizopo na kubakiza zile za kisera, huku akionyesha kusikitishwa na hoja ya upungufu mkubwa wa watumishi inayojirudia mara kwa mara.
"Mathalani kwenye sekta ya elimu tuna upungufu wa walimu asilimia 51, pia kwenye jumla ya kata zetu zote 21 tuna maafisa kilimo wachache sana wasiozidi 12", alisema Digha.
Social Plugin