MWANAFUNZI CHUO KIKUU CHA IRINGA AUAWA KWA KUNYONGWA NA MPENZI WAKE


Mwanafunzi Petronila Mwanisawa aliyeuawa
***
Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Prudence Patrick (21) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Iringa mkazi wa Semtema Iringa ,mwenyeji wa mkoa wa Kagera kwa tuhuma za kumnyonga mpenzi wake Petronila Mwanisawa (22) ambaye pia ni mwanafunzi katika chuo hicho, mkazi wa Semtema Iringa chanzo kikielezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, amesema tukio hilo limetokea Juni 2, mwaka huu maeneo ya Kihesa mkoani Iringa ambapo taarifa za awali za upelelezi zinaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi baina ya marehemu na mtuhumiwa na kwamba wote walikuwa wanafunzi katika Chuo Kikuu Iringa.

"Juni 2, 2021 majira ya saa 12 jioni, maeneo ya Semtema Kata ya Kihesa Manispaa na Mkoa wa Iringa, Petronila Pascal Mwanisawa miaka 22 ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa zamani Tumaini na mkazi wa Semtema alifariki dunia, baada ya kunyongwa shingo na mpenzi wake mwanafunzi mwenzake wa chuo hicho aitwaye Prudence Patrick miaka 21 mkazi wa Semtema Kihesa.

"Kabla ya tukio hilo Juni 1, 2021 saa 12 jioni marehemu alifika nyumbani kwa mtuhumiwa pamoja na rafiki yake aitwaye Belnada Njafula kwa lengo la kuchukua pesa yake shilingi 5000/= ambayo alikuwa anamdai mpenzi wake huyo ambapo marehemu alibaki peke yake nyumbani kwa mtuhumiwa kwa muda ili alipwe deni hilo, baada ya rafiki aliyeongozana naye kuondoka kwa ajili ya majukumu mengine.

"Hata hivyo, marehemu hakurudi nyumbani kwao mpaka pale mwili wake ulipokutwa ndani ya chumba cha mtuhumiwa umefungiwa ndani na umelazwa kitandani ukitokwa na povu mdomoni na damu puani.

"Taarifa za awali za upelelezi zinaonesha kuwa, chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa mapenzi baina ya marehemu na mtuhumiwa ambaye amekamatwa na upelelezi wa tukio bado unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kujibu mashtaka yanayomkabili,"amesema Kamanda Bwire.

Kamanda Bwire amesema, siku ya tukio marehemu hakurudi nyumbani kwao jambo ambalo si kawaida yake, hivyo wazazi wake waliingiwa na hofu na kuanza kumtafuta.

"Marehemu alikuwa anaishi na wazazi wake, na huyu mtuhumiwa yeye alikuwa amepanga. Kwa hiyo siku ya tukio alitoka kwenda chuo, lakini mpaka usiku akawa hajarudi, ndipo wazazi walianza kupata wasiwasi, wakampigia simu rafiki yake lakini hawakufanikiwa,"ameeleza.

"Kwa hiyo jana ndiyo tukampata, na hiyo ni baada ya mtuhumiwa mwenyewe kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa mzazi wa marehemu akisema alikuwa na Petronela na kwamba amefariki dunia. Baada ya hapo hakupatikana tena,"amesema.

Pia amesema, baada ya wazazi kupata taarifa hizo waliripoti kituo cha polisi, ndipo askari walikwenda katika nyumba ya mtuhumiwa na kuukuta mwili wa marehemu.

"Mtuhumiwa tulimkamata njia ya kuelekea Dodoma alipokuwa akijaribu kutoroka na upelelezi wa tukio hilo unaendelea,"ameongeza.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Bwire, wanafunzi hao walikuwa wanasomea fani ya uandishi wa habari chuoni hapo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post