Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia kijana kwa tuhuma za kumuua shangazi yake Lamina Samwebe (65) mkazi wa Ngamanga Misheni katika kata ya Ipinda wilayani Kyela kwa kumcharanga mapanga akimtuhumu kuwa ni mchawi na amekuwa akimroga asipate maendeleo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei amesema jina la kijana huyo limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama na anadaiwa kufanya mauaji hayo Juni 22,2021 kwa kumvamia shangazi yake huyo akiwa amelala nyumbani kwake saa 5:45 usiku kisha akatekeleza unyama huo.
"Kijana huyo alimkata na panga shangazi maeneo ya kichwani, shingoni na vidole vitatu vya mkono wa kulia na kwamba bibi huyo alikosa msaada kutokana na kuishi peke yake kwenye nyumba hiyo.
Baada ya kupata taarifa, askari walifika katika eneo la tukio na kukuta shangazi yake akiwa amekufa chumbani kwake, walipofuatilia walimkuta kijana huyo akiwa na panga ambalo alilitumia kwenye mauaji hayo na ndipo wakamtia mbaroni", amesema Kamanda Matei.
Social Plugin