Waziri wa mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefungua Mnada wa Magena uliopo katika halmashauri ya mji wa Tarime mkoani Mara uliokuwa umefungwa kwa zaidi ya Miaka kumi ambapo ameagiza kuanza haraka kwa Mnada huo huku akiwataka wakurugenzi wa Halmashauri kupunguza Tozo kwa wafanyabiashara wa mifugo katika Minada kutokana na kuwepo kwa Tozo lukuki inayopelekea Minada Mingi kufungwa.
Waziri Wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametoa kauli hiyo jana akiwa ameongozana na Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Mhe. Michael Kembaki pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi na uchukuzi Mwita Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini katika kufungua Mnada wa Magena uliopo katika halmashauri ya Mji wa Tarime Mkoani Mara uliokuwa umefungwa kwa zaidi ya Miaka kumi.
Akitoa maelekezo ya Serikali mara baada ya kuufungua Mnada huo, Waziri Wa Mifugo Mhe. Ndaki amesisitiza suala la tozo lukuki kwa wafanyabiashara wa Mifugo hali ambayo inapelekea Minada mingi ya mifugo kufungwa ambapo amewalekeza Wakurugenzi wa halmashauri kupunguza tozo hizo.
Aidha Mhe. Ndaki amewataka Wananchi wa Tarime kutumia fursa hiyo kujinufaisha kiuchumi huku akiagiza kupangwa Siku maalumu ya mnada ili mnada huo uanze haraka kupokea mifugo kutoka maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Tarime Mjini Mhe. Michael Kembaki ametoa Pongezi kwa Waziri wa Mifugo na uvuvi kwa kusikiliza kilio chake na kuamua kuambatana naye kwa ajili ya kufungua Mnada wa magena hali ambayo itafungua Fursa kwa wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini katika kukuza uchumi.
Aidha Mhe. Kembaki amewaomba wananchi kutumia Vyema Fursa hiyo ya Mnada wa Magena kunufaika kiuchumi.
“ Nimekuwa nikimsumbua Mhe. Waziri wa Mifugo kwa ajili ya Mnada huu wa Magena ambao umekwama hapa kwa muda Mrefu ,nitumie fursa hii kumpongeza Mhe. Waziri kwa kunisikiliza na leo hii tumeambatana kuja hapa kuufungua mnada huu rasmi. Niwaombe Wananchi wa jimbo langu la Tarime Mjini kutumia fursa hii ya mnada huu kukuza uchumi”, amesema Kembaki
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na uchukuzi Mhe. Mwita Waitara ambaye Pia ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini amemshukuru Waziri wa Mifugo na Uvuvi mashimba Ndaki kwa kumsikiliza Mhe. Kembaki Mbunge wa jimbo la Tarime Mjini kwa kufika na kufungua Mnada wa Magena ambao ulikuwa umefungwa kwa muda Mrefu.
Aidha Mhe. Waitara amewataka wananchi kuacha kupeleka Mifugo aina ya ng’ombe nchi Jirani ya Kenya badala yake watumie Mnada wa Magena kwa ajili ya kujinufaisha kiuchumi.
Mnada wa Magena umefunguliwa rasmi Tarehe 12 June 2021 ikiwa ni baada ya kufungwa kwa kipindi cha muda mrefu hali ambayo iliwalazimu wananchi wa jimbo la Tarime Mjini na maeneo mengine kupelekea mifugo yao nchi jirani ya Kenya.