Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIKU YA MTOTO WA AFRIKA IWE CHACHU YA MAPAMBANO DHIDI YA VVU & UKIMWI KWA WATOTO


Mratibu wa shughuli za ukatili wa kijinsia kutoka AGPAHI, Dkt. Jane Kashumba (kulia) akizungumza na waelimisha rika.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Leo Juni 16 Tanzania inaungana na mataifa mengine kimataifa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo chimbuko lake ni kumbukumbu ya watoto zaidi 2000 waliouawa wakati wakiandamana kupinga ubaguzi wa rangi katika mfumo wa elimu nchini Afrika Kusini mnamo mwaka 1976.

Katika kuadhimisha siku hii, waelimisha rika kupitia Klabu za watoto kutoka kwenye kliniki za huduma za dawa na matunzo zinazosimamiwa na asasi inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia, Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) ,wanashauri jamii kulinda watoto kwa kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.

Waelimisha rika hao wanasema njia pekee ya kulinda watoto wa Afrika ni kuwaepusha dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa kuhamasisha kupima afya zao na kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za kufubaza makali ya VVU, hivyo siku hii ya Mtoto wa Afrika iwe chachu ya mapambano hayo.

Muelimisha rika,Eva Alex, kutoka Lubaga, Shinyanga anashauri pia watoto na vijana wanaoishi na maambukizi ya VVU kushiriki katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI kwa kujiepusha na tabia hatarishi ikiwemo kuepuka ngono zisizo salama na matumizi ya dawa za kulevya.

“Tunapoadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika nguvu kubwa tuielekeze katika kuwalinda watoto dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI lakini pia kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wanaosafirishwa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kwa ajili ya kufanya kazi za ndani, kilimo na mifugo kwani wengi wao bado hawajajua njia za kukabiliana na vitendo vya ukatili”, amesema Eva.

“Pia elimu ya VVU na UKIMWI iendelee kutolewa katika jamii ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya kondomu na wananchi wapime afya zao mara kwa mara na walio kwenye mahusiano wajue hali za afya zao kabla ya kuoana na pindi wanapobainika kuwa wana maambukizi ya VVU basi waanze kutumia dawa mara moja, pia kwa wajawazito waweze kumkinga mtoto atakayezaliwa na maambukizi ya VVU”,ameongeza.

Aidha amesema ni vyema watu wanaoishi na maambukizi ya VVU wazingatie matumizi sahihi ya ARV’s badala ya kuacha ili kuzuia makali ya VVU.

Naye Coletha Martine, kutoka Ndala, Shinyanga ameshauri watoto kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe bora ili kujenga mwili na kuimarisha afya na kusaidia dawa za ARV’s kufanya kazi vizuri ili kukabiliana na magonjwa nyemelezi.

“Watoto kupitia klabu za watoto zinazosimamiwa na AGPAHI wanapewa elimu kuhusu “Afya ya Uzazi na Lishe Bora” na kushauriwa namna ya kupata vyakula vyenye lishe ikiwa ni pamoja na kuhamasisha na kuwawezesha kwa mafunzo ya ufugaji wa kuku na kilimo cha mboga mboga”,amesema Coletha.

Katika hatua nyingine, ameiomba serikali iwape kipaumbele watoto na vijana kwa kuwapa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia huku akiwasihi wazazi na walezi kuwa na taarifa za kutosha juu ya watoto wao wanaosafirishwa kwenda kufanya kazi za ndani,kilimo na ufugaji mbali na maeneo ya nyumbani.

Kwa upande wake Mratibu wa shughuli za ukatili wa kijinsia kutoka AGPAHI, Dkt. Jane Kashumba amesema AGPAHI inaendelea na mipango ya kuwafikia watoto wengi zaidi ili kuwapima afya zao na kuwaweka kwenye huduma ili kukabiliana na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.

“Licha ya kwamba bado watoto wengi hawajafikiwa na mipango ya upimaji afya, sisi tunaendelea kuwafikia watoto kupitia vituo vya afya pindi wazazi wao wanapofika kupata huduma”,amesema Dkt. Jane.

Amesema pia AGPAHI inafuatilia watoto waliopo katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU na UKIMWI kupitia kwa waelimisha rika waliopewa mafunzo na AGPAHI ambao wamekuwa wakitoa elimu ya VVU na UKIMWI.

Kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2021 ni "Tutekeleze Agenda 2040 kwa Afrika inayolinda Haki za Mtoto".

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com