WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 Madiwani, Maafisa Tarafa, na Watendaji wa Kata kote nchini watapata posho zitakazowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao muhimu katika jamii.
Waziri Nchemba amesema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2021/2022 na kueleza kuwa baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwaelekeza kuangalia namna ya kutatua changamoto za watendaji hao wamekuja na masuluhisho ambayo yatarahisisha utendaji kazi wa viongozi hao.
Kwa upande wa madiwani, Waziri Nchemba amesema kuwa wawakilishi hao wanafanya kazi nzuri ya kusimamia shughuli za maendeleo licha ya baadhi ya Halmashauri kuwakopa posho zao, jambo ambalo Rais Samia amesikia kilio chao na kutoa maelekezo kwa kushirikiana na TAMISEMI kutafutia ufumbuzi suala hilo na amependekeza kuanzia mwaka wa fedha 2021/ 2022 Serikali ianze kulipa posho za kila mwezi kwa waheshimiwa Madiwani kupitia akaunti zao kwa halmashauri zenye uwezo mdogo kimapato na halmashauri 16 zenye uwezo mkubwa kimapato (daraja A,) zitaendelea kutumia mapato yake ya ndani kulipa posho za madiwani kupitia kwenye akaunti zao.
Kwa upande wa Maafisa Tarafa ambao ni viunganishi muhimu wa ngazi ya kata na Wilaya na hufanya kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali, kwa kutambua umuhimu wao Serikali iliwapa pikipiki za kurahisha majukumu yao, Hata hivyo wengi wao wanashindwa kugharamia ununuzi wa mafuta na matengenezo na kulazimika kuwachangisha wananchi na kuomba msaada kwa wadau mbalimbali.
"Kupitia hotuba hii napenda kuwajulisha Maafisa Tarafa wote nchini kuwa Mama yetu amesikia kilio chenu hivyo napendekeza kuanzia 2021/2022 Serikali kuu ianze kulipa posho ya shilingi laki moja kwa kila Afisa Tarafa ili waweze kumudu gharama za mafuta na matengenezo." Amesema.
Aidha kwa upande wa watendaji wa Kata ambao ni wasimamizi wa kazi za sekta zote na watendaji wakuu wa Kata wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu katika Kata ikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato na masuala ya usalama na wengi wao hutumia mishahara kufanya kazi mbalimbali ikiwemo ufuatiliaji wa mapato ya Serikali kwa kukodi pikipiki, Niwaeleze kuwa Mama yetu, Rais Samia amesikia kilio hiki na kutuelekeza kutafuta ufumbuzi, napendekeza kuanzia 2021/ 2022 Serikali kuanza kulipa posho ya shilingi laki moja kwa mwezi kwa kila mtendaji Kata kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri yaliyokuwa yakitumika kulipa madiwani.
Social Plugin