Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SINGIDA WAANZA KUKUSANYA MAPATO YA MAEGESHO KWA MFUMO MPYA WA KIELEKTRONIKI


Mkuu wa Mkoa wa Singida Binilith Mahenge akizungumza  kabla ya kuzindua  Mfumo mpya  wa kielektoniki wa ukusanyaji mapato kupitia maegesho ya vyombo vya moto.

 Na Edina Alex, Singida.

MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amezindua  mfumo mpya wa kielektroniki ujulikanao kama "TARURA e-REVENUE MANAGEMENT INFORMATION SYSTEM" kwa ajili ukusanyaji mapato  ya maegesho ya vyombo vya moto mkoani Singida.

Dkt. Binilith amezindua mfumo huo leo wakati akifungua kikao cha kuwajengea uwezo  viongozi juu ya matumizi ya mfumo huo wa ukusanyaji mapato ya maegesho ya vyombo vya moto, matumizi ya hifadhi za barabara pamoja na tozo za adhabu kutokana na ukiukwaji wa matumizi ya hifadhi za barabara yanayosimamiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA).

Alisema kuanzishwa mfumo huo utaenda kuleta  ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya serikali  yatakayosaidia  maboresho  na maendeleo ya miundombinu ya barabara,kupunguza kero ya kudaiwa  ushuru kwa kuwa mtumiaji atalipa  kwa kutumia simu ya mkononi ,wakala  ama matawi ya benki ya NMB na CRDB.

"Binafsi naona mfumo huu utaleta tija kubwa  katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na utoaji huduma kwa  wananchi", alisema Dkt. Mahenge.

Aidha Dkt. Mahenge  aliutaka wakala huo kuhakikisha  elimu ya mfumo huo inafikishwa kikamilifu kwa wananchi ili wote wawe na uelewa wa pamoja  na kuepusha malalamiko kwa watumiaji.

Alitoa wito pia kwa  wananchi kuyapokea mabadiliko hayo na kulipa wao wenyewe ushuru wa maegesho ili kuepuka tozo ama faini zisizo za lazima.

Akifafanua namna ya ufanyaji  kazi wa mfumo huo  Mhasibu kitengo Cha mapato TARURA makao makuu, Osward Mobily alisema mteja anaweza kulipia ushuru wa maegesho kwa saa ,siku,wiki au mwezi. Pia  mteja anaweza kuomba mwenyewe kumbukumbu namba  ya malipo kwa ajili ya kufanya malipo ya kabla ya ushuru wa maegesho kwa kupiga *152*00#.

Singida ni mkoa wa pili kuzindua mfumo huu ukitanguliwa na Mkoa wa Iringa, ambapo imeelezwa kuwa kama utasimamiwa na kutumika vizuri utaleta tija kwa ustawi wa miundombinu ya barabara zinazozunguka mkoani Singida.
Mtaalamu wa Kitengo cha mapato kutoka TARURA Makao Makuu Osward Mobily akifafanua jinsi ya kufanya malipo kwa mfumowa TeMIS. Picha zote na Edina Alex
Mratibu wa TARURA Mkoa wa Singida William Boniphance akizungumza kwenye uzinduzi huo
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kyaratu akichangia hoja ukumbini
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM)Mkoa wa Singida Lucy Shee  akichangia hoja kwa ajili ya maboresho ya mfumo huo.
Mrakibu wa Polisi (SP) Nyangi Choma akichangia.
Mchambuzi wa Mifumo kutoka Makao Makuu ya TARURA, Joseph Chigalula akieleza jinsi ya kufanya malipo ya ushuru wa maegesho kwa kutumia mfumo huo mpya.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida Alhaj Juma Kilimba akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mkutano ukiendelea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com