Mwananchi akitumia simu
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Dhana ya uhuru wa kutoa na kupata taarifa bado haijaeleweka miongoni mwa Watanzania walio wengi. Zipo nadharia mgongano juu ya maana halisi ya uhuru huo. Wapo wanaoamini uhuru wa kutoa na kupata taarifa una mipaka yake na wengine wakisisitiza uhuru huo haupaswi kuwekewa mipaka yoyote.
Hata hivyo, katika muktadha wa nchi zinazoendelea kama Tanzania, ni muhimu kujielekeza katika maana ya uhuru wa kutoa na kupata taarifa wenye wajibu. Hii ina maana kwamba, haki ya kutoa na kupokea taarifa inaathiriwa na vikwazo chanya kadha wa kadha vikiwemo usalama wa raia na nchi, faragha ya mtu binafsi, utu wa mtu, na imani za kidini.
Ingawa hakuna utafiti wa dhahiri uliofanyika kujua kiwango cha uelewa na matumizi sahihi ya vyombo na majukwaa mbalimbali ya upashanaji taarifa, bado wengi wao wana uelewa duni kuhusu usahihi wa taarifa wanazopokea, kuzitumia na kuzisambaza. Aidha, uelewa hafifu wa sheria na taratibu za upashanaji taarifa na mmomonyoko wa maadili umechangia ongezeko la matumizi holela ya majukwaa mbalimbali hususan mitandao ya kijamii katika kusambaza taarifa zisizo sahihi.
Ripoti mbalimbali zinathibitisha ongezeko la watumiaji wa simu za kiganjani waliojisali kutumia huduma za kampuni za simu nchini ni zaidi ya milioni 50, na zaidi ya milioni 27 wameunganishwa na mtandao wa intaneti.
Aidha, matumizi ya majukwaa binafsi ya upashanaji taarifa mtandaoni kama vile Facebook, Instagram, and Twitter yameshamiri miongoni mwa watanzania wa rika na kipato tofauti. Pia, idadi ya vyombo na majukwaa ya kihabari mtandaoni imeongezeko ambapo Ripoti ya TCRA inayoishia Agosti 2020 imeonesha kwamba kuna TV za mtandaoni 352, radio za mtandaoni 45, blogu 110, na majukwaa ya mtandaoni 8.
Ukuaji huu umepanua wigo kwa raia kutoa na kupata taarifa ingawa zipo changamoto kadhaa za kisheria zinazodumaza uhuru huu. Kwa upande mwingine, ongezeko hili limeongeza changamoto nyingi hususan kuhusu matumizi sahihi ya njia hizi za kupeana taarifa.
Kumekuwepo na upazaji sauti wa kuondolewa kwa vipengele vya sheria na kanuni vinavyokwamisha uhuru wa wananchi kupashana taarifa.
Hata hivyo, bado kuna changamoto kubwa miongoni mwa raia wenyewe wa kutoelewa aina gani ya taarifa waisambaze, watumie, wakati na madhara au faida zitakazojitokeza kupitia taarifa husika.
Mfano, matukio kadhaa yameripotiwa ya matumizi yasiyofaa ya majukwaa ya upashanaji taarifa ikiwemo picha za utupu, uhamasishaji wa tabia zisizofaa kama utumiaji wa madawa ya kulevya, wizi na biashara ya ngono. Matukio haya yanaongeza mmomonyoko wa maadili hususan miongoni mwa vijana.
Aidha, kumekuwepo na ongezeko la usambazaji wa taarifa za uzushi zenye nia ovu miongoni mwa raia wenyewe au dhidi ya taasisi na viongozi wa serikali na binafsi. Kwa bahati mbaya, watanzania walio wengi hawana weledi sahihi wa kupambanua taarifa ya kweli na uzushi ni ipi. Hii imewapelekea wengi wao kutenda kosa la kusambaza taarifa za uongo.
Kwa muktadha huu ipo haja ya serikali kupitia taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na watetezi mbalimbali wa haki ya kutoa maoni na kupata taarifa nchini ikiwemo MISA Tanzania kuwekeza nguvu zaidi katika kutoa elimu sahihi kwa umma juu ya matumizi sahihi ya vyombo na majukwaa ya upashanaji taarifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Dr. Hassan Abbas ni miongoni mwa wadau wanaohimiza utekelezaji wa uhuru wa kutoa na kupata taarifa wenye uwajibikaji. Haki na uhuru wa kutoa maoni na kupata taarifa utakuwa na maana tu endapo wananchi watapata uelewa sahihi juu ya utekelezaji wa haki hii ya kikatiba.
Social Plugin