UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NA MATARAJIO YA UONGOZI WA AWAMU YA SITA YA SERIKALI YA TANZANIA


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Uhuru wa vyombo vya habari ni miongoni mwa haki za msingi za kila raia wa Tanzania. Haki hii huwawezesha raia kupata na kutoa taarifa, kujieleza ili kutoa maoni yao katika masuala mbalimbali yenye maslahi yao. 

Pia, uhuru wa vyombo vya habari huchochea kukua kwa misingi ya haki za binadamu, demokrasia, na utawala bora.

 Kuwepo kwa misingi hii husaidia wananchi kushiriki katika uendeshaji wa nchi, kuchagua viongozi wanaowataka, kuhoji uendeshaji wa serikali pamoja na kufahamu masuala yanayoathiri maisha yao.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na changamoto zinazoathiri au kuminya uhuru vya vyombo vya habari. Taasisi na asasi za kiraia zikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA TAN), LHRC, na zinginezo zimeripoti matukio kadhaa kuashiria kuwepo kwa mazingira magumu kwa vyombo vya habari na wanahabari kutekeleza uhuru huu.

 Matukio hayo ni pamoja na kufutwa au kufungia vyombo vya habari, kutoza faini na karipio dhidi ya vyombo vya habari, ukamataji na uwekaji kizuizini kwa waandishi wa habari na vikwazo vya kisheria na kikanuni zinazodhibiti vyombo vya habari na wanahabari kutekeleza wajibu wao kwa uhuru.

Hata hivyo, kuapishwa kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Awamu ya Sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunaleta matumaini ya kuwepo kwa mazingira wezeshi yanayohimiza uhuru wa vyombo vya habari nchini.

 Matumaini haya yanajikita katika nia thabiti ya Mhe. Rais Samia ya kuhakikisha vyombo vya habari vinatimiza wajibu wake wa kuhabarisha umma kwa uhuru.

Akizungumza wakati wa kikao chake na wahariri wa vyombo vya habari kilichoafanyika tarehe 28 June 2021, Mhe. Rais Samia alinukuliwa akihimiza vyombo vya habari vilivyofungiwa kufunguliwa huku akivitaka kuzingatia sheria na miongozo ya serikali. 

Aidha, Mhe. Rais Samia mbali ya kuelekeza kulindwa na kuheshimiwa kwa uhuru wa vyombo vya habari, alitoa hakikisho la serikali yake kuzingatia kuwepo kwa sheria zisizokwaza upatikanaji na usambazaji wa habari nchini.

Ni matumaini ya wanahabari nchini kwamba Mhe. Rais Samia ameonesha dhamira ya wazi ya kuweka mazingira mazuri yanayochagiza uhuru wa vyombo vya habari. 

Hata hivyo, ni wajibu wa kila chombo cha Habari na waandishi wa Habari kuutumia vizuri uhuru huu kwa kutimiza Wajibu kwa kuzingatia weledi na maadili katika kutafuat, kuchakata na kusambaza taarifa na habari mbalimbali zenye maslahi kwa umma.

 Daima watambue kwamba hakuna uhuru bila wajibu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post