Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAAFISA UTUMISHI MNAO WAJIBU WA KUWAELIMISHA WATUMISHI ILI WAWEZE KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO IPASAVYO


KATIBU wa Tume ya Utumishi wa Umma Bwana Nyakimura Muhoji (aliyevaa shati katikati) katika picha ya pamoja na Maafisa wa Tume walioshiriki katika kupokea na kusikiliza kero, malalamiko na changamoto za kiutendaji kutoka kwa watumishi wa umma na wadau Wilaya ya Kisarawe-Pwani tarehe 16-18 Juni 2021 katika kuadhimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2021. (picha na PSC).

                                                  ***

Maafisa Utumishi wamekumbushwa wajibu wao wa kuwaelimisha na kutoa mafunzo kwa watumishi, si kwa watumishi wapya tu bali kwa watumishi wote ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bwana Nyakimura Muhoji amesema haya jana Wilayani Kisarawe, Pwani katika mahojiano maalum wakati alipokutana na Maafisa wa Tume waliokuwa Kisarawe kupokea, kusikiliza na kutafutia ufumbuzi changamoto za kiutendaji za kiutumishi katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021  inayoendelea kufanyika.

“Maafisa Utumishi kila mmoja mahali pake pa kazi anao wajibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi  kuhusu Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo, Nyaraka na Maelekezo halali yanayotolewa. Wana wajibu pia  wa kutoa mafunzo na kujielimisha masuala ya kiutumishi si kwa watumishi wapya tu, bali kwa watumishi wote ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri” alisema.

Bwana Muhoji alisema jukumu la kutoa elimu kwa watumishi wa umma kuhusu masuala ya Kiutumishi ni la Maafisa Utumishi na Wakuu wa Idara za Rasilimali watu katika Taasisi za Umma, hivyo ni muhimu sana kuwa na  utaratibu wa kukutana mara kwa mara na watumishi.

“Maafisa Utumishi mnapaswa kukutana kuelimishana nini mnatakiwa kufanya, waelezeni pia watumishi nini wanatakiwa kufanya. Waraka wa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya upo, utumieni na ufanyieni kazi. Wanapowafuata watumishi wajibuni kwa lugha ya staha, tumieni lugha nzuri katika kuwahudumia watumishi wenu, msipowashughulikia matatizo yao watumishi kunapelekea malalamiko”, alisema Muhoji.

Akizungumzia kuhusu kusoma nyaraka mbalimbali, Bwana Muhoji alisema kuwa ni muhimu sana Watumishi wa Umma kuzisoma, kuzielewa na kuzitekeleza ipasavyo nyaraka mbalimbali. Alisema, Maafisa utumishi wanapaswa wakati wote wanapotekeleza kazi zao, wakarejea nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Serikali wakati wa kushughulikia masuala ya watumishi.

Alitoa wito kwa Maafisa Utumishi na Viongozi kuwa tayari wakati wote kusikiliza na kuyashughulikia kwa wakati masuala ya kiutumishi yanayowasilishwa na Watumishi wa Umma.


                                                  Imetolewa na:  

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Tume ya Utumishi wa Umma.

KISARAWE- PWANI

18 Juni, 2021



 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com