BALOZI MULAMULA AKUTANA NA MKURUGENZI MTENDAJI WA BENKI YA DUNIA KANDA YA AFRIKA


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo ofisini kwake jijini Dodoma.

Waziri Mulamula amesema mazungumzo yake na Dkt. Taufila ambaye pia alikuwa anajitambulisha yamelenga kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Tanzania ili kuimarisha mahusiano hayo na hivyo kunufaika na miradi ya maendeleo.

Akiongelea uhusiano baina ya Tanzania na Benki ya Dunia Mhe. Balozi Mulamula amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha mahusiano kati ya Tanzania na Benki hiyo yanaimarika na kuendeleza uwezo wa Watanzania wanaosimamia miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na kuendeleza sekta binafsi na kuifanya kuwa imara.

“leo hapa tumejadiliana juu ya mahusiano yetu, kuangalia namna ya kuyaboresha ili kunufaika na miradi  ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki hiyo, kuwajengea uwezo watu wetu wanaosimamia utekelezaji wa miradi hiyo na uimarishaji wa Sekta binafsi ili kuwa imara na hivyo kufikia maendeleo ya kweli,” alisema Balozi Mulamula

Akiongelea kuhusu mipango ya Serikali ya kuimarisha Sekta Binafsi Mhe Waziri Mulamula amemuhakikishia Dkt. Taufilo nia na mtizamo wa Serikali wa kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza nchini ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi hasa ikizingatiwa kuwa Benki ya Dunia inachukulia sekta binafsi kama chachu ya maendeleo na hivyo kuwa na miradi ya kusaidia ukuzaji wa Sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji huyowa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo amesema miongoi mwa mambo waliyojadili leo ni pamoja na umuhimu wa kuhusisha sekta binafsi na kuiendeleza.

Amesema miongoni mwa vipaumbele vya Benki ya Dunia kwa sasa ni kuimarisha Sekta binafsi na kuifanya kuwa imara hasa katika maeneo ya biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, na ukuzaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuiwezesha duniani kuendelea kufanya shughuli zake hasa katika kipindi hiki cha changamoto ya ugonjwa wa Covid 19.

Amesema wamekubaliana kuendelea kushirikiana na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Benki hiyo na hivyo kuiwezesha Tanzania kunufaika na miradi ya maendeleo inayosimamiwa na benki hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post