Baraza la madiwani halmashauri ya Wilaya ya Busega limetaka uwepo wa Mahakama ya Wilaya Busega. Hayo yamesemwa na wajumbe wa baraza hilo wakati wa kikao cha baraza la madiwani robo ya tatu lililofanyika tarehe 04 Juni 2021 ukumbi wa Silisos.
Diwani kata ya Nyasimo Mhe. Mickness Mahela amehoji kuhusu suala la uwepo wa Mahakama wilayani Busega, akisema kwamba imekuwa kero kubwa kwa wakazi wa Busega wanapotaka kupata huduma ya mahakama, kwani inawalazimu kwenda Wilaya jirani ya Bariadi kupata huduma hiyo.
“Wilaya ya Busega ina takribani miaka tisa kwasasa, hivyo uwepo wa mahakama ni muhimu kwa wananchi wetu” aliongeza Mhe. Bi. Mickness Mahela. Wajumbe wa baraza hilo wamekiri kwamba uwepo wa mahakama ni suala lisilopingika, huku wakidai kwamba wilaya inahitaji mahakama ili kuondoa kero ya wakazi na wananchi wa Busega.
Akitoa ufafanuzi wa suala la uwepo wa mahakama wilayani Busega, mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa wilaya Busega Bw. David Pallangyo anasema kwamba ni suala ambalo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imekua ikifuatilia kwa ukaribu na inaendelea na ufutiliaji. Kwa upande mwingine ameeleza kwamba licha ya watumishi wa mahakama kupangiwa kufanyia kazi zao wakiwa Busega lakini bado wanafanyia kazi zao wilayani Bariadi.
Aidha, hoja ya matengenezo ya magari iliibuliwa na wajumbe huku wakitaka uwepo wa gereji ya halmasuri ili kuwa na ufanisi wa matengenezo ya magari hayo kuliko kupeleka magari hayo kwa Wakala wa Ufundi wa Umeme na utengenezaji wa Magari ya Serikali (TEMESA). Akitoa ufafanuzi wa suala hilo Mkurugenzi Mtendaji Bw. Anderson Kabuko licha ya changamoto ya TEMESA, lakini tayari marekebisho na matengenezo madogo yanafanyika kwa baadhi ya magari na kazi hiyo inafanywa na fundi wa halmashauri.
Suala la stendi ya Wilaya ambayo imeanza kufanya kazi mwanzoni mwa mwezi wa tano mwaka huu, pia limepata wasaa wa kujadiliwa na baraza hilo. Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Kabuko amesema tayari halmashauri imevunja mkataba na mkandarasi wa awali ambae alikuwa akijenga stendi hiyo kutokana na kutofikia ubora wa ujenzi, na tayari utaratibu unafanyika ili kumpata mkandarasi mwingine. Baraza hilo limetaka ujenzi wa wa stendi hiyo uboreshwe hasa njia za kupita magari ili kuondoa usumbufu na kero.
Akiahirisha kikao cha baraza hilo, Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe, ametaka kuendelea kwa juhudi ujenzi wa stendi ya Wilaya, na kuagiza kwamba kwasasa hatuhitaji mkandarasi, mhandisi wa ujenzi kwa kushirikiana na Meneja wa TARURA kufanya kazi ya ujenzi kuendelea na ujenzi wa stendi ya Wilaya, Nyashimo. Kwa upande mwingine ameomba viongozi wa mkoa kufuatilia suala la mahakama ili wilaya ya Busega iweze kupata mahakama.
Social Plugin