BASHE AAGIZA RAS TABORA KUWAONDOA WATUMISHI WA MANISPAA YA TABORA WALIOCHUKUA MASHAMBA SKIMU INALA
الأربعاء, يونيو 30, 2021
NA TIGANYA VINCENT
NAIBU Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amemwagiza Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu kuwaondoa watumishi wote wa Manispaa ya Tabora ambao wamejimilikisha mashamba katika mradi wa Umwagiliaji wa Inala.
Alisema wamechukua maeneo hayo na kusababisha wananchi wanaozunguka mradi huo kukosa mashamba kwa ajili ya kulima kilimo cha mpunga.
Bashe alitoa kauli hiyo jana wakati wa kufungua maadhimisho ya sherehe za siku ya Ushirika Duniani (SUD) ambapo Kitaifa inafanyika Mkoani Tabora na kilele kitakuwa tarehe 3 Julai mwaka huu.
Alisema licha ya Serikali kutumia fedha nyingi kujenga Bwawa hilo bado mradi huo haufanyikazi vizuri kama ulivyokusudiwa kwa sababu ya watumishi wa Manispaa ya Tabora kujimilikisha mashamba ambayo hawayalimi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo alimwagiza Mrajis wa Vyama Vya ushirika Nchini Dkt. Benson Ndiege kufanya miaka mitatu mfululizo maadhimisho ya sherehe za siku ya Ushirika Duniani (SUD) katika Mkoa mmoja badala ya kila mwaka kuanga katika eneo jipya.
Alisema hali hiyo itasaidia kuleta matokeo chanya kutokana na Washirika kujifunza katika eneo mmoja kwa kipindi cha miaka mitatu.
Wakati huo Naibu Waziri amewataka vijana kujiunga na ushirika ili kuondoa dhana potofu kuwa Ushirika na wazee na watu waliochoka.
Alisema ushirika ndio silaha pekee itakayowasaidia wakulima kupanga katika masoko na kupata bei nzuri itakayowasaidia kuondoa katika umaskini.
Bashe alisema Serikali itaendelea kuunga mkono Ushirika ili hatimaye uweze kuwa msaada mkubwa kwa wakulima kuchangia katika pato la Taifa kutoka la sasa la asilimia 26 na kuongezeka Zaidi.
Alisema kilimo ndio Sekta inayotoa ajira kwa wananchi wengi ni vema ikachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la Taifa.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya ushirika Duniani mwaka huu ni Ushirika pamoja tujijenge uya kwa ubora na tija.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin