Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA DUNIA YAAHIDI KUISAIDIA TANZANIA KUKABILIANA NA ATHARI ZA CORONA


Na. Peter Haule na Josephine Majula, WFM, Dodoma
Benki ya Dunia (WB) imefungua dirisha kwa Tanzania la kusaidia kukabiliana na athari za ugonjwa wa Uviko 19 katika Sekta mbalimbali ikiwemo ya Utalii, biashara na bajeti ya Serikali.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji anayeziwakilisha Nchi za Kundi la Kwanza la Afrika katika Benki ya Dunia (AfG1 Constituency), Dkt. Taufila Nyamadzabo.

Dkt. Nchemba alisema kuwa ugonjwa wa Uviko 19 umekuwa na athari katika Bajeti ya Serikali kwa ujumla, kwa kuwa, kunapotokea changamoto za kiuchumi katika nchi zinazofanya biashara na Tanzania huathiri makusanyo ya kodi zinazotokana na uagizwaji na uingizaji wa bidhaa pamoja na mapato yatokanayo na ufanyaji wa biashara na nchi nyingine.

“Licha ya ahadi ya Benki ya Dunia kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na athari za Uviko 19, Benki hiyo imeahidi kufungua miradi iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu ukiwemo mradi wa kuboresha miundombinu ya elimu ya Sekondari nchini, jambo ambalo ni la faraja kwa Taifa kwa kuwa ni eneo ambalo tunalipa kipaumbele”, alieleza Dkt. Nchemba.

Aidha ameeleza kuwa mambo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na mwenendo wa Mfumuko wa Bei kwa Tanzania ambao umeendelea kuwa kati ya asilimia 3 hadi 5, Deni la Taifa ambalo ni himilivu ambapo deni la Serikali kwa uwiano wa Pato la Taifa ni asilimia 27.9 ili hali ukomo ni asilimia 70 kwa kutumia vigezo vya Shirika la Fedha la Umoja wa Mataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB), pamoja na mchango wa Benki ya Dunia katika kuweizesha Sekta Binafsi nchini.

Pia ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia kwa kuidhinisha mikopo minne ya masharti nafuu yenye jumla ya dola za Marekani bilioni 1.017 (sawa na shilingi trilioni 2.3391) kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni ya kuboresha miundombinu ya barabara, kuimarisha mazingira ya ufundishaji na mafunzo katika taasisi za elimu ya juu, kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma bora za umeme visiwani Zanzibar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Taufila Nyamadzabo, ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za maendeleo na kupunguza umasikini. Pia amesema kuwa Serikali inatakiwa kuendelea kukusanya rasilimali kwa ajiri ya kukabiliana na athari za Uviko 19 na pia kutumia rasilimali hizo kikamilifu katika kutekeleza miradi ikiwemo inayotolewa fedha na WB na kuishirikisha Sekta Binafsi katika miradi ya maendeleo ili kuajiri vijana wengi zaidi.

Pia ameahidi kuwa ataendelea kusimama kwa niaba ya Serikali ya Tanzania katika kuiwakilisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa WB ili kunufaika kwa ushirika wake na Benki ya Dunia, hususan katika uidhinishaji wa fedha za miradi ya maendeleo.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com