Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amefanya kikao cha utambulisho na watumishi wote wa CCM wa Makao Makuu Dodoma.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 4 Juni, 2021 Makao Makuu ya CCM Dodoma katika Ukumbi wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.
Pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu ametilia mkazo kuendelea kusimamia Katiba, Kanuni, Taratibu, na Utamaduni wa Chama ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji ndani ya Chama.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu ameeleza kuanza kwa utekelezaji wa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika Hotuba yake katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa cha tarehe 30 Aprili, 2021, aliyoelekeza kushughulikiwa kwa changamoto mbalimbali za watumishi wa CCM ikiwemo malimbikizo ya madeni pamoja na maslahi mengine.
Aidha, asubuhi ya leo Katibu Mkuu amemtembelea Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Bara Mzee Samwel Malecela na kufanya naye mazungumzo Nyumbani kwake Mtaa wa Kilimani Dodoma ikiwa ni muendelezo wa Katibu Mkuu kukutana na wazee wastaafu mbalimbali kwa lengo la kujifunza na kujitambulisha.
Katika hatua nyinginie, Jioni ya leo Katibu Mkuu ametembelewa na vijana wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Naibu Spika na Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt. Tulia Akson, ambapo Katibu Mkuu pamoja na mambo mengine amewasisitiza vijana kuendelea kutafuta maarifa ili kujiandaa na fursa zilizopo na zijazo.
Imetolewa na;
Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)